Azam FC yapewa mbinu za kuwafunga Triangle FC

Muktasari:

  • Azam FC imepewa mbinu ya namna ya kwenda kushinda dhidi ya Triangle FC ya Zimbabwe ambayo ni kushambulia kipindi cha kwanza ili kuwachanganya wenyeji wao.

KIPA Deogratius Munishi 'Dida' alikuwa jukwaani wakati Azam FC inacheza na Triangle ya Zimbabwe mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ametoa la moyoni kuelekea mchezo wa marudiano.

Azam FC ilipoteza nyumbani kwa bao 1-0 dhidi ya Triangle FC katika mchezo wao wa marudiano Septemba 28, Dida amewapa ushauri wa bure kwamba wakazitumie dakika 45 za kipindi cha kwanza kupata mabao mawili.

Azam FC itaondoka kuwaifuata Triangle FC kwa makundi mawili, msafara wa kwanza utakuwa Septemba 22 chini ya kocha msaidizi Idd Cheche na wapili utakuwa 23 na kocha mkuu Etienne Ndayiragijje.

Dida amesema Azam FC inaweza kufanya maajabu ugenini lakini kwa kukitumia kipindi cha kwanza kwa malengo ili cha pili kikawe cha kulinda ushindi wao.

"Inawezekana Azam FC kwenda kushinda ugenini, kwanza wapinzani wao watakuwa wanaona wamemaliza kila kitu baada ya kushinda ugenini, hilo likawe njia kwao kuwachanganya na kasi"

"Triangle FC wakiwachanganya na kasi ya kushambuliwa ndio itakuwa siri ya Azam FC kupata ushindi, wasikate tamaa bado wana nafasi kubwa, naungana na anachosema kocha kwamba inawezekana kwenda kushinda ugenini"amesema.