Simba SC yaichapa Azam yapaa kileleni, Namungo, Alliance zatakata Ligi Kuu Tanzania Bara

Muktasari:

Mshambuliaji Kagere ameweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyefunga kila mechi aliyocheza hadi sasa akiwa amefunga mabao saba katika michezo sita iliyocheza Simba.

Dar es Salaam. Mshambuliaji Meddie Kagere amefunga bao lake la saba msimu huu akiongoza Simba SC kuichapa Azam kwa goli 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kagere mfungaji bora wa msimu uliopita alifunga bao hilo pekee katika dakika 49, akiunganisha kwa kichwa krosi ya Francis Kahata na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa Simba.

Mshambuliaji Kagere ameweka rekodi ya kuwa mchezaji pekee aliyefunga kila mechi aliyocheza hadi sasa akiwa amefunga mabao saba katika michezo sita iliyocheza Simba.

Kagere sasa anahitaji kufunga mabao 16 katika mechi 31 zilizobaki za ligi ili kuifikia rekodi yake ya mabao 23 aliyofunga msimu uliopita.

Katika mabao 11 yaliyofungwa na Simba hadi sasa Kagere amefunga saba akifuatiwa na Miraj Athumani mwenye mabao matatu.

Ushindi huo unaifanya Simba kuendeleza rekodi yake ya kushinda mechi tano mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara na kufikisha pointi 15, kileleni, huku Azam ikipoteza rekodi yake ya kutokufungwa.

Katika dakika 45 za kipindi cha kwanza timu hizo zilitoka suluhu.

Licha ya Simba kufanya mashambulizi kupitia pembeni, lakini mashuti ya washambuliaji, Kagere na Sharaf Shiboub na kiungo, Mzamiru Yassin yaliokolewa na safu ya ulinzi ya Azam ikiongozwa na kipa, Mwadini Ali.

Dakika ya 35, Mashabiki wa Simba walitegemea kupata bao la kuongoza kwa penati baada ya Mzamiru aliyekuwa kwenye muvu kuanguka kwenye box lakini mwamuzi, Hance Mabena alikataa, akionyesha ishara ya kuwa sio penalti.

Azam ilifanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Simba lakini mashuti ya Frank Domayo, Chirwa na Daly Djodi yaliokolewa na safi ya ulinzi ya Simba.

Ajibu aibua shangwe Taifa

Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Patrick Aussems dakika ya 87 kwa kumuingiza mshambuliaji Ibrahim Ajibu kuchukua nafasi ya Francis Kahata yaliibua shangwe kwa mashabiki wa Simba.

Nyota huyo aliyejiunga na Simba msimu huu akitokea kwa watani zao Yanga katika dakika chache alizoingia aligusa mpira mara tano.

Awali alicheza mpira dakika ya 89 na kupiga krosi kwa Kagere, dakika ya 90 alichezewa faulo akiwa amekabwa na Bruce Kangwa, Salum Abubakar, Iddy Seleman na Donald Ngoma ambao walishindwa kumnyang'anya mpira.

Mpira mwingine aliocheza Ajibu ni pasi ya Gerson Fraga ambayo alimrudishia na kuingia nao kwenye 18, lakini beki wa Azam akamshika akiwa katika harakati za kupiga shuti, ingawa mwamuzi Hance Mabena alionyesha ishara ya kukataa kuwa sio faulo.

Mpira wa mwisho aliocheza Ajibu ni shuti nje kidogo ya 18 lakini likamgonga beki wa Azam na kurudi uwanjani.

Ushindi wa bao 1-0 umetawala kwenye viwanja vinne tofauti kati ya saba katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara 'VPL' ambayo imeendelea kutimua vumbi leo.

Namungo, Alliance zatakata

Wekundu wa Msimbazi, Simba wameendelea kujikita kwenye kilele cha msimamo wa Ligi hiyo, baada ya kuifunga Azam bao 1-0, lililofungwa na Meddie Kagere.

Bao la Kagere, limeifanya Simba kufikisha pointi 15 huku wakifuatiwa na Namungo wenye pointi 13, leo, wameifunga Mtibwa Sugar bao 1-0, lililofungwa na Bigirimana Braise kwenye uwanja wa Majaliwa, Lindi.

Alliance ya Mwanza, wakiwa nyumbani kwenye  uwanja  Nyamagana, waliifunga Ruvu Shooting bao 1-0 huku Polisi Tanzania nao wakiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mwadui ya Shinyanga.

Shujaa kwa upande wa Polisi Tanzania wakiwa uwanja wa Ushiriki, Moshi alikuwa Baraka Majogoro aliyefunga bao pekee lililowafanya kusalia na pointi tatu nyumbani.

Matokeo mengine, Maafande wa Tanzania Prisons wameshindwa kuitambia Biashara United ya Mara kwa kulazimishwa suluhu kwenye uwanja wao wa Sokoine, Mbeya.

Coastal Union ya Juma Mgunda na wenyewe walilazimishwa suluhu wakiwa Mkwakwani, Tanga na Singida United. Ndanda ya Mtwara walitoka sare bao 1-1 na Lipuli ya Iringa.