Makame afunguka kuhusu picha zinazosambaa, tumehama nyumba hatujafukuzwa

Muktasari:

Alitaja gharama ya nyumba ambayo Yanga iliwalipia ni 4 milioni, ambapo sasa wametafuta nyumba nyingine nzuri ambayo gharama yake ni nafuu zaidi.

PICHA zinazunguka kwenye mitandao ya jamii zikiwaonyesha wachezaji wa Yanga wakihamisha vitu vyao kutoka kwenye nyumba waliyokuwa wanaishi, Kariakoo jijini Dar es Salaam lakini taarifa ikasambaa kuwa jamaa hao walitimuliwa.

Picha hizo, zinawaonyesha, Abdulaziz Makame, Adeyum Saleh, Mapinduzi Balama na wengine.

Mwanaspoti lilimpata Makame na akasisitiza hawakufukuzwa isipokuwa waliamua wenyewe kuhama. Kiungo huyo mrefu alisema, hawakufurahishwa na mazingira pamoja na kodi kubwa waliyokuwa wanaitoa.

“Mkataba wetu na Yanga ilikuwa kulipiwa miezi sita na ilipoisha, tuliamua wenyewe kuondoka kwa sababu kodi iliyokuwa inalipwa na klabu ni kubwa tofauti na uhalisia wa nyumba yenyewe na sisi hatuna uwezo wa kuilipa ndio maana tumehama kwenda kwenye nyumba tunayoweza kumudu kulipa kodi,”alisema Makame.

Hata hivyo, wakati Makame anajibu suala hilo, alikuwa kwenye presha ya mchezo ambapo jana Jumatano Yanga ilikuwa inacheza mechi ya Kombe la FA dhidi ya Gwambina FC.

Alitaja gharama ya nyumba ambayo Yanga iliwalipia ni 4 milioni, ambapo sasa wametafuta nyumba nyingine nzuri ambayo gharama yake ni nafuu zaidi.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema; “Kilichotokea ni jambo la kawaida ambalo kila mtu analifanya, wachezaji wenyewe waliamua kutoka hapo walipokuwa wamepangiwa na klabu na kwenda kuishi mahali pengine.”