Msuva: Morocco ukikutwa nje unazurura kuna mambo matatu yanaweza kukutana nayo

Dar es Salaam. Hakuna mwenye kuthubutu kati ya Saimon Msuva au Nickson Kibabage wa Difaa El Jadida ya Morocco kutoka nje kipindi hiki cha kampeni nchini humo ya kupunguza maambukizi ya virusi vya Corona.

Ukikutwa nje unazurura bila mpango kwa mujibu wa Msuva kuna mambo matatu yanaweza kukutana nayo ambayo ni kipigo kama cha mbwa koko, faini na kifungo.

"Kabla ya kuchukuliwa maelezo cha kwanza huwa ni kipigo, maelezo utakayoyatoa ndio yanaweza kukufanya utozwe faini peke yake au wakuweke na rumande kwa muda fulani.

"Wapo siriazi sana, wale ambao wamekuwa wakaidi tumekuwa tukiona wakitandikwa kupitia vipande vya video ambao tumekuwa tukitumiana wachezaji kwa njia ya WhatsApp, " alisema Msuva.

Upande wake Kibabage alisema kinachoweza kumwokoa mzurulaji akiwekwa mtu kati na watu wa usalama ni mbio zake, "Kama unambio kushinda polisi basi unaweza kuzurula.

"Lakini pamoja na yote tunapaswa kufuata maelekezo ya Serikali ili kuwa sehemu ya kupunguza maambukizi ya virusi hivi hatari," alisema kinda huyo