ABC yatakata Ligi ya Kikapu Dar

Muktasari:

  • Robo ya tatu ABC wakiwatumia wachezaji wake wakongwe Gilbert Batungi,Philbert Mwaipungu waliwabana wapinzani kila eneo,

Dar es Salaam. Uzoefu wa wachezaji wa ABC jana uliwawezesha kuibuka na ushindi wa pointi 76-45 dhidi ya Mgulani [JKT] katika mchezo wa Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA) iliyoanza jana kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa.

Katika mchezo huo timu zote mbili zilianza taratibu na dakika moja kabla robo ya kwanza kumalizika, ABC ilikuja juu na kufunga pointi za haraka haraka na kuongoza 13-11.

Robo ya pili ilianza kwa Mgulani kubadilika kucheza pasi za haraka haraka huku wakimtumia zaidi Claud Msheni aliyekuwa anaisumbua ABC muda wote.

Hadi Mapumziko Mgulani JKT iliongoza kwa pointi 30- 21.

Robo ya tatu ABC wakiwatumia wachezaji wake wakongwe Gilbert Batungi,Philbert Mwaipungu waliwabana wapinzani kila eneo,

ABC ilitumia nafasi hiyo na kufunga pointi 30-6 iliyowashangaza wapenzi wengi waliokuwepo uwanjani hapo kutokana na idadi ya pointi nyingi zilivyofungwa.

Robo ya nne ilipoanza ABC waliendeleza makali na kufanikiwa kufunga pointi 25-9 dhidi ya Mgulani JKT.

Katika mchezo huo Alinani Andrew wa ABC aliongoza kwa kufunga pointi 24,kati ya pointi hizo aliweza kufunga katika maeneo ya mitupo mitatu mara tano.

Aliyemfuatia alikuwa Philbert Mwaipunga aliyefunga pointi 15 wakati kwa upande wa Mgulani walikuwa ni Dadi Salimu 13 na Claudi Msheni 14 .

Katika mchezo huo Gilbert Batungi wa ABC alidaka mipira ya rebounds mara 10 akifuatiwa na Alinani Andrew aliyedaka mara nane.