Ah! Kumbe tatizo Simba, Yanga

Muktasari:

  • Juzi Jumatano, Manara kupitia ukurasa wake wa Instagram alionyesha kushangazwa na ratiba kuipa nafasi Yanga kucheza mechi 11 mfululizo za Ligi Kuu Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Kilio cha Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara juu ya watani wao wa jadi Yanga kucheza mechi 11 mfululizo jijini Dar es Salaam kinatoa ishara ya hofu ya klabu yake inayojiandaa na mechi baina ya timu hizo, Septemba 30.

Juzi Jumatano, Manara kupitia ukurasa wake wa Instagram alionyesha kushangazwa na ratiba kuipa nafasi Yanga kucheza mechi 11 mfululizo za Ligi Kuu Dar es Salaam.

“Haijawahi kutokea kokote duniani toka Ulimwengu umeumbwa, klabu moja kucheza mechi 12 mfululizo kwenye kituo chake. Usisahau JKT, Simba, KMC na African Lyon zitachezewa Taifa. Hoja hapa ni nini?” Alihoji Manara. Mechi 11 mfululizo ambazo Yanga itacheza jijini ni dhidi ya Stand United, Coastal Union, Singida United, JKT Tanzania, Simba, Mbao FC, Alliance, KMC, Lipuli, Ndanda na African Lyon.

Ingawa Manara ameonekana kuzinyooshea kidole mechi 11 za Yanga zitakazochezwa hapa jijini, mchezo baina ya timu hizo mbili kongwe unaonyesha dalili kuwa ndio chanzo cha malalamiko hayo tofauti na michezo mingine 10 iliyobaki.

Ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara inaiweka katika wakati mgumu Simba kujiandaa na mechi hiyo huku ikiwatengenezea mazingira mazuri watani wao Yanga kupata maandalizi mazuri kabla ya kuvaana kwenye Uwanja wa Taifa.

Uamuzi wa Bodi ya Ligi kutobadili tarehe ya mchezo wa watani wa jadi kama ilivyotarajiwa, unaweza kupokewa vyema na Yanga ambao ratiba inawapa nafasi ya kucheza mechi hiyo ikiwa imepata muda wa kutosha kujiandaa kulinganisha na Simba.

Timu hiyo italazimika kufanya kazi ya ziada kujiandaa na Yanga kwa kuwa kabla ya hapo italazimika kusafiri umbali mrefu kwenda mikoani kucheza mechi tatu mfululizo kati ya minne kabla ya kukutana na Yanga tofauti na watani wao ambao kabla ya mechi hiyo watacheza jijini.

Wakati Yanga ikibaki jijini kucheza na Stand United, Coastal Union, Singida United, JKT Tanzania kabla ya kuivaa Simba, watani wao watakuwa wanasafiri umbali wa zaidi ya kilomita 2865 katika miji tofauti nchini ambako watakwenda kucheza mechi za ligi kabla ya kurejea jijini kuikabili Yanga.

Simba ambayo iko Mtwara ilikotua kwa ndege jana asubuhi kucheza mechi ya kesho dhidi ya Ndanda, baada ya mchezo huo italazimika kusafiri umbali wa kilomita 1708 hadi Mwanza ambako itacheza na Mbao FC, Septemba 20 na baadaye itasafiri kilomita 168 kutoka Mwanza kwenda Shinyanga kupepetana na Mwadui, Septemba 22.

Baada ya hapo Simba itasafiri umbali wa kilomita 1011 kutoka Mwadui hadi Dar es Salaam ambapo itakuwa na mchezo dhidi ya Biashara United, Septemba 27 na itakuwa na siku mbili tu za maandalizi kabla ya kuvaana na Yanga.

Hata hivyo, mambo yanaweza kugeuka mzunguko wa pili kwa kuwa Yanga italazimika kutoka nje ya Dar es Salaam kwenye idadi kubwa ya mechi jambo linaloweza kuinufaisha Simba endapo itacheza vyema karata zake.

Simba pia ni wanufaika wa ratiba hiyo kwa sababu watacheza mechi nane mfululizo jijini baada ya kumaliza mechi zake za ugenini dhidi ya Ndanda, Mbao na Mwadui.

Ikimalizana na Biashara United na Yanga, mechi nyingine sita mfululizo ambazo Simba itacheza hapa jijini ni dhidi ya African Lyon, Alliance, Ruvu Shooting, JKT Tanzania na KMC.

Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura alisema ratiba haina tatizo. “Ukitazama utagundua Mkoa wa Dar es Salaam kuna timu kama tano ambazo zikicheza na Yanga au Simba zinatumia Uwanja wa Taifa au Uhuru ambazo ni African Lyon, Ruvu Shooting, JKT Tanzania na KMC.

“Kutokana na hilo, vyovyote ambavyo ratiba ingepangwa bado mechi hizo zingechezwa Dar es Salaam tu na ratiba imekuwa na uwiano mzuri kwa timu kucheza mechi za nyumbani na ugenini,” alisema Wambura.

Ofisa Habari wa Yanga, Dismas Ten alionyesha kushangazwa na wanaolalamika kuhusu ratiba kuipendelea klabu hiyo.

“Siyo mechi zote Yanga ndio tutakuwa wenyeji wa mchezo. Michezo mingine tutakuwa ugenini na watu wanapaswa kukumbuka kuwa wanaopanga ratiba ni Bodi ya Ligi,” alisema Ten.

“Mchezo wa Simba dhidi ya Yanga upo na utachezwa siku iliyopangwa kama kawaida na mashabiki wajitokeze kushabikia timu zao kwenye siku hiyo,” alisema Ofisa Habari wa TFF Clifford Ndimbo.

Ndimbo alisema katika mchezo huo wamezidisha ulinzi wa kutosha ili kutoa fursa kwa idadi kubwa ya mashabiki kujitokeza kwenda kuzishuhudia timu hizo kongwe nchini zikitoana jasho. Simba ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kombe walilotwaa msimu uliopita.