Ajibu alianzisha , Yanga yajipanga

ACHANA na harakati za usajili zinazoendelea kuhusiana na fundi wa Yanga, Ibrahim Ajibu ambaye hivi karibuni amewashtusha mashabiki baada ya jina lake kukatwa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Sasa unaambiwa kuna ishu mpya ambayo itawapa mzuka mashabiki wa Jangwani.

Kuna mipango mizito inaendelea kuhusiana na usajili wa Ajibu, ambaye anakaribia kumaliza mkataba wake pale Yanga, anadaiwa kuwindwa na mabingwa watetezi, Simba wakati mabosi wa Yanga wakipambana kumpa mkataba mpya kutokana na uwezo wake na jinsi anavyolibeba chama lake.

Hata hivyo, mzuka zaidi ni kuwa Ajibu aliyekosa mechi iliyopita dhidi ya Lipuli na Yanga kutokana na kusumbuliwa na na nyonga na timu yake ikachapwa kidude na Kamwene, sasa amepona na amenza mazoezi na wenzake.

Katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Samora mjini Iringa, Yanga ilifungwa bao 1-0 na sasa inajiandaa na mechi ya Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC au Kombe la FA) katika hatua ya robo fainali dhidi ya Alliance mechi itakayochezwa Machi 28, mwaka huu, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Ajibu, ambaye anatajwa kusaini mkataba wa awali Simba ambayo ni timu yake ya zamani, aliwaongoza wenzake 19 jana Alhamis katika mazoezi yaliyofanyika Uwanja wa Polisi Kurasini, Dar es Salaam.

Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh alisema nyota 20 wakiwa chini ya Kocha Msaidizi, Noel Mwandila wameanza mazoezi na Ajibu ndiye aliyekuwa mchezaji wa kwanza kufika mazoezini kutokana na nafasi yake huku akielezwa amezikana inshu za kutaka kutua Msimbazi.

Saleh alisema kikosi hicho kinachoundwa na nyota 30 kinawakosa wachezaji tisa ambao wanne kati yao wapo katika majukumu ya Timu za Taifa ‘Taifa Stars’ na watano wanasumbuliwa na majeraha yanayowafanya wakae nje ya timu hadi hapo daktari atakapothibitisha kurudi kwao uwanjani.

“Tunaendelea na mazoezi kama kawaida kujiandaa na mchezo wetu wa Kombe la FA dhidi ya Alliance ni wachezaji 20 wanaoendelea na mazoezi wengine wapo Stars na wale majeruhi wamepewa muda wa mapumziko kwaajili ya kuendelea kujitibia.

“Juma Abdul, Juma Mahadhi, Haji Mwinyi, Abdallah Shaib ‘Ninja’, Mohamed Issa ‘Banka’, Endrew Vincent ‘Dante’ hawa wana matatizo tofauti, Kelvin Yondani, Feisal Salum, Gadiel Michael wapo na timu ya taifa na Ramadhani Kabwili ameitwa Timu ya Taifa U-20,” alisema.

Saleh alisema nyota wote waliopo mazoezini bado hawajaanza kambi wanatokea nyumbani na kujiunga pamoja mazoezini na kuweka wazi kuwa wataingia kambini siku mbili kabla ya kusafiri kuelekea Mwanza lengo likiwa ni kuwakusanya nyota wote waliokuwa Stars ili kufanya mazoezi ya pamoja kabla ya kukutana na Alliance.

Alisema wanawaheshimu wapinzani wao na ndio maana wameanza kujiandaa mapema na wanaamini katika mchezo huo wanakila sababu ya kupata matokeo ili kujitengenezea mazingira ya wao kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa.

“Majeruhi yanatutesa lakini tunaamini hadi Machi 28 nyota wetu watakuwa wamerejea kikosini na kujifua kwa ajili ya mchezo huo ambao ni muhimu sana kwetu kupata matokeo ili tuweze kuingia hatua inayofuata,” alisema.

Yanga yajipanga upyaaa

Wakati timu hiyo ikiwa inajiandaa kuikabili Alliance pale CCM Kirumba jijini Mwanza, Kocha Mwandila alisema baada ya mapumziko wachezaji wake sasa wameanza rasmi kusaka dawa ya kuimaliza Alliance ili kupata matokeo mazuri na kuwawezesha kusonga mbele hatua ya nusu fainali ili kuwinda tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa mwakani.

“Kufungwa na Lipuli hakuna maana kwamba wachezaji wetu wameondoka ndani ya mstari, kilichotokea walipata nafasi wakaitumia sisi tulikosa utulivu wa kufunga ila kimbinu tulikuwa vizuri.

“Tunaijua Alliance ilivyo na kasi na ina vijana wengi wadogo, tunajipanga kwani Kombe la FA linatoa nafasi kwa bingwa kushiriki michuano ya kimataifa.

“Kiu kubwa ya Wanayanga ni kuona klabu yao mwakani inashiriki michuano ya kimataifa, tutapambana kuhakikisha tunafikia malengo na matumaini yao,” alisema.