Ali Kiba awafanyia 'saprize' Wazenji

Saturday September 28 2019

 

By SALOME GREGORY

MSANII wa muziki wa Bongo fleva Ali Kiba jana Ijumaa usiku alitumbuiza nyimbo zake pendwa zisizozidi sita katika mgahwa wa 6 Degrees South katika hafla iliyoandaliwa kwa lengo la kuwaburudisha wateja wao na wadau wa burudani.
Hafla hiyo ilikua maalumu kwa baadhi ya watu na uwepo wa Ali Kiba haukutangazwa kabla ilikua ni zawadi ya ghafla kwa wageni waalikwa wa hafla hiyo iliyohudhuriwa na waalikwa zaidi ya 100 ambao walijumuisha viongozi wa serikali, wanachama wa sekta binafsi na watu maarufu ndani na nje ya nchi.
Msanii huyo ghafla alitokea upande wa VIP na kuelekea moja kwa moja jukwaani na  kupelekea ukumbi kulipuka kwa kelele za furaha huku akiwa na uso wa tabasamu alisalimia mashabiki wake na kuanza kutumbuiza wimbo wake wa Seduce Me.
“Habari zenu, nina furaha kuwa mbele yenu maana Zanzibar ni nyumbani. Wote tufurahi pamoja na kucheza usiku wa leo (jana),” alisema Kiba akiwa jukwaani.
Mashabiki katika hafla hiyo walipewa nafasi ya kuchagua wimbo mmoja baada ya mwingine na kisha Kiba kutumbuiza kulingana na matakwa ya mashabiki wake na muda ulipofika wa kushuka jukwaani alilazimika kuondoka huku mashabiki wakihitaji burudani zaidi.
Akizungumza katika hafla hiyo mmiliki wa mgahawa huo, Saleh Said alisema ni jukumu lao kutoa huduma bora zaidi kwa wateja wao na kuwafanya wafurahie huduma za mgahawa wao huo.
“Kwa sababu hiyo nilimualika Ali Kiba kuja kutuburudisha hapa ili kufanya shughuli hii kuwa adhimu  zaidi. Tulipopanga kufanya sherehe hii, nilizungumza na ZMMI na Vodacom walilipokea vizuri na kuwa tayari kudhamini, tunawashukuru kufanikisha vyema shughuli hii, tunasherehekea mafanikio yetu na wadau wetu wote kiujumla,” alisema Said.
Katika vivutio vya mji kongwe wa Stone Town, mgahawa wa 6 Degrees South ni kivutio kikubwa kwa wengi. Sehemu tulivu inatazamana na Bahari ya Hindi. Katika kusherekea miaka sita tokea ilipofunguliwa na inaendelea kuboresha huduma zake na kuwa mojawapo ya mgahawa maarufu visiwani.


Advertisement