Alliance wajipanga kupindua meza kwa Yanga

Muktasari:

Katika michezo minne waliyokutana tangu Alliance imepanda ligi kuu yote Yanga imeweza kupata ushindi yote jambo ambalo limefanya wababe hao wa eneo la Mahina jijini Mwanza kuwa vibonde kwa mabingwa hao wa kistoria.

ALLIANCE FC imesema haitaki tena kuwa vibonde wa Yanga hivyo wameweka mikakati kuhakikisha wanawafunga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaopigwa kesho Jumamosi jijini Dar es Salaam.
Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Mathias Wandiba amesema sasa nao wanataka kuonja ushindi katika mchezo huo ambao wamejipanga kuhakikisha wanapata pointi tatu za kwanza kutoka Yanga.
Alisema haiwezekani katika michezo minne waliyokutana nao yote wamepoteza jambo ambalo nao sasa wanataka kupata furaha kwa kuwafunga kwenye pambano hilo.
“Tunataka kupindua meza haiwezekani kila mchezo tutakaokutana na Yanga watufunge hivyo tumekuja kwa nguvu zote kuhakikisha tunaondoka na pointi tatu za kwanza kutoka kwao," alisema Wandiba.
Alisema kikosi chao kipo sawa katika mchezo huo ambapo wanajua wapi kwa kuwabana Yanga wasifurukute hivyo hawana presha kikubwa wataingia kwa tahadhari kubwa kupata ushindi kwani wanacheza na timu kubwa.
Katika michezo minne  tangu Alliance wapande daraja waliyokutana mitatu ya ligi kuu na mmoja wa kombe la FA, Yanga imeshinda mechi zote.
Msimu uliopita walishinda 3-0 mchezo wa mzunguko wa kwanza kisha raundi ya pili wakashinda bao 1-0, mchezo wa kombe la FA waliwafunga Alliance kwa mikwaju ya penalti ya 4-3 baada ya ndani ya dakika 90 kutoka sare ya bao 1-1.
Msimu huu mzunguko wa kwanza Yanga walishinda bao  2-1 mchezo uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.