Ambokile alichakaza viatu, sasa anakula kiyoyozi cha ndege TP Mazembe

Muktasari:

  • “Nimechekwa, nimebezwa na kuambiwa ‘wewe dogo huwezi kucheza mpira unapoteza muda wako nenda katafute kazi nyingine ya kufanya’, moyo uliniuma ila sikuwaonyesha, nikiangalia maisha yao kwa sasa wao ndio wapo hovyo na wengine hawana ujasiri wa kunitazama usoni nikikutana nao hivi sasa,” anasema.

BILA uvumilivu, kupambana na kusimamia ndoto zake, Eliud Ambokile angeisikia TP Mazembe kwenye redio tu. Unaambiwa jamaa licha ya kukumbana na kejeli nyingi na kukatishwa tamaa kwamba mguu wake sio dhahabu kwenye soka, aliziba masikio.

Ambokile kutoka kutembea kwa mguu umbali mrefu katika kusaka mkate wake hadi kuziona ndege ni usafiri wa kawaida kwake, anasisitiza alisota sana, lakini uvumilivu ndio uliombeba.

Mwanaspoti limefanya mazungumzo na mchezaji huyo anayekipiga TP Mazembe kwa sasa na amefunguka mengi ikiwamo elimu yake na namna alivyokwama kwenda Chuo Kikuu.

Kama kuna kitu anakizingatia Ambokile ni kutomdharau mtu kwenye maisha yake na anabainisha kuwa amepitia kuchekwa na kukatishwa tamaa na kwamba waliofanya hivyo wengi wao ndio wanaoishi maisha ya tabu.

“Nimechekwa, nimebezwa na kuambiwa ‘wewe dogo huwezi kucheza mpira unapoteza muda wako nenda katafute kazi nyingine ya kufanya’, moyo uliniuma ila sikuwaonyesha, nikiangalia maisha yao kwa sasa wao ndio wapo hovyo na wengine hawana ujasiri wa kunitazama usoni nikikutana nao hivi sasa,” anasema.

MAISHA YAKE YA SOKA KADI 2

Tangu aanze kucheza soka, Ambokile anasema amewahi kupata kadi mbili za njano akiwa na timu ya Mbeya City dhidi ya Njombe Mji na Prisons, kutokana na mchezo kuwa na ushindani wa hali ya juu.

“Nakumbuka nilipata kadi hizo kipindi nilichokuwa nafunga sana, jicho la mabeki wa upinzani lilikuwa linanitazama kwa makini, iliniumiza kwani niliona kama nachafua CV yangu,” anasema.

WACHEZAJI WALIOMPONDA

Msimu wa 2017/18 alijiunga rasmi na Mbeya City. Akiwa hapo, anafichua namna ambavyo alikumbana na maneno ya karaha kutoka kwa wachezaji waliokuwa na namba ndani ya kikosi cha kwanza.

Anasema alishangazwa na kauli za wachezaji wenzake kumwambia bila kificho kwamba hawezi kucheza wala kupata namba wakimtaka akatafute kazi ya kufanya na sio soka.

“Siwezi kuwataja majina licha ya kwamba waliniumiza sana moyo ingawa haikuwa sababu ya kunitoa kwenye reli kupigania ndoto zangu na niliongeza bidii,” anasema.

Anasimulia alivyopambana kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza na akawa tegemeo wa kufunga mabao kabla ya kuondoka kwenda TP Mazembe akiwa amefunga 10.

“Maisha ni safari ndefu, nimejifunza kuheshimu kila ninayemuona mbele yangu kwani siwezi kujua Mungu amemkusudia nini, sijafika kirahisi TP Mazembe nilivumilia changamoto za hapa na pale,” anasema.

Anasema maisha yake yalianza kufunguka taratibu ikiwamo kuitwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23, mwaka 2017 kucheza michuano ya Cosafa. “Tulicheza nyumbani kisha tulisafiri kwenda Burundi.

“Hapo ndio ilikuwa mara yangu ya kwanza kupanda ndege, nilipata nguvu ya kujiamini zaidi kwamba nitafanya makubwa kwenye soka, niliepuka kuishi kwa akili za watu ambao wananikatisha tamaa,” anasema.

MCHONGO WA TP MAZEMBE

Anasimulia namna alivyonasa dili la kuchezea TP Mazembe kwamba ilikuwa ni kama zali tu na kwa kuwa lililopangwa na Mwenyezi Mungu ni lazima litimie, alipigiwa simu na viongozi wa klabu hiyo Jamhuri ya Kidemokrasiaya Kongo wakimueleza kwamba wamekuwa wakimfuatilia mambo yake anayoyafanya uwanjani na kwamba wanahitaji huduma yake. Fasta wakafanya mazungumzo na wakala wake na dili likatiki.

“Wakala akanipigia simu kwamba kuna dili la kuichezea TP Mazembe akaniuliza je nipo tayari, nikamjibu nipo tayari, makubaliano yakafanyika nikasaini mkataba wa miaka mitatu,” anasema straika huyo.

MAISHA YA TP MAZEMBE

Kitu kikubwa alichokitaja Ambokile alichokiona ni cha tofauti na Tanzania ni namna Shirikisho la Soka la Congo, linavyohusika kuweka mazingira mazuri kwa wachezaji ili wapate dili za kucheza Ulaya.

“Shirikisho la mpira wa miguu Congo, lina mikakati maalumu ya kuandaa wachezaji wa kucheza Ulaya ndio maana wachezaji wao wengi wapo nje, sijaliona hilo kwa TFF yetu,” anasema.

CHAKULA CHA WACHEZAJI WA TP MAZEMBE

Anasema asilimia kubwa ya wachezaji wa TP Mazembe wanapendelea kula ugali, samaki na kuku. Wali anasema ni mara chache sana. “Wanapenda ugali, hiyo inakuwa ni mchana na usiku, wakibadili tena wa nadra ni tambi na wali ila mboga ni zile zile,” anasema.

STAREHE YAO KUBWA

Anasema suala la ulevi kwa wachezaji wa Congo ni kitu cha kawaida na kwamba kama wametoka mapumziko na wamerudi na ‘hengiova’ basi kocha hatoi mazoezi magumu.

“Kuna wakati kocha anasema wazi kwamba wachezaji bado wana pombe kichwani anawafanyisha mazoezi kidogo anawaruhusu wakapumzike ila anawasisitiza siku inayofuata kuwa vizuri, uzuri wao ni waelewa,”

“Kuhusu starehe ya wanawake hilo sijaliona tofauti na jinsi ambavyo wanasemwa wachezaji wa Tanzania, huku ni kama wanaheshimu sana mahusiano ustaa hauwafanyi watumie kwa anasa,”anasema.

KAMBI HUWA VIJIJINI

Anasema mmiliki wa TP Mazembe, Moses Katumbi amejenga kambi za timu kijijini ambako hakuna mambo mengi na inapofikia wakati wa kwenda kucheza mechi wanarudi mjini.

“Kwanza usafiri wao mkubwa ni ndege kutokana na miundo mbinu yao, ndio maana imekuwa rahisi kutoka kijijini kwenda mjini kucheza mechi, mazoezi yao ni magumu ya kumuweka mchezaji fiti,” anasema.

WANAPENDA MIKOROGO

Ambokile anasema si jambo la ajabu kuwaona wachezaji wa Congo wanajichubua. Hiyo imekuwa ni kama ni utamaduni wao “Wanapenda kupendeza sana, kujichubua sio kwa wanawake tu bali hata wachezaji wanapaka mafuta makali,” anasema.

ANAJIONA KWENYE KIKOSI CHA KWANZA?

Anasema si kazi rahisi kuanza moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza ingawa anaamini kadri siku zinavyokwenda atapata nafasi ya kuanza na kuaminiwa.

“Kikosi cha TP Mazembe kina ushindani kuanzia wanaoanza na wale ambao wanakaa benchi, kikubwa kocha anakuwa ananiweka benchi hiyo ni hatua kubwa kwangu, naamini kinachofuata nitaanza,” anasema.

KIDIABA BABA LAO

Anasema kipa wa zamani wa timu hiyo, Robert Kidiaba ambaye kwa sasa ndiye Waziri wa Michezo wa nchi hiyo, amekuwa faraja akiwapambania kuhakikisha wanafuata nyayo za Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.

“Kitendo cha kujua tumetoka Tanzania anatuona ni ndugu zake, amekuwa akituelekeza namna ya kuvumilia bila kukata tamaa akituambia hata Samatta hakuanza moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza.

“Anatuambia tukiwa na tatizo lolote tuwe tunamwambia ili ajue namna ya kutufanya tujisikie ni watu muhimu kwenye timu, ajabu ana nidhamu kubwa na anajishusha licha ya kuwa ni waziri, tunamuona kama baba yetu,” anasema.

MASHABIKI MAZEMBE

Anasema kuna haja kwa timu za Tanzania kuwa na mashabiki ambao wanacheka pamoja na timu na wanalia pamoja na timu, kitu alichokiona kwenye klabu ya TP Mazembe.

“Mashabiki wakiwa uwanjani wanachukulia kama kazi, hata timu ikipoteza hawakati tamaa kushangilia kwa nguvu, hilo linakuwa linazichanganya timu pinzani, kifupi wanajitoa kwa moyo, hao wana haki kuitwa mchezaji wa 12,” anasema.

SANAMU YA SAMATTA YAGEUZWA UTALII

Ufalme wa Mbwana Samatta katika nchi ya Congo, unakuwa siku hadi siku, anasema sanamu yake kwa sasa wameigeuza kama sehemu ya kwenda kufanya utalii.

“Wakijua umetoka Tanzania nchi aliyozaliwa Samatta basi unapata heshima kubwa kwa Wakongo, watu wanakwenda kupiga picha na sanamu yake.

“Wanamuombea kila kheri waliposikia anatua Aston Villa, natamani Watanzania wangejua namna mtu huyu anavyoheshimika Congo, utadhani kiongozi mkubwa serikalini mbele ya mashabiki,” anasema.

Anasema kuna wakati mwingine mashabiki wanakuwa wanamuimba kwenye mechi zao licha ya kwamba hayupo tena kwenye timu. “Hata Thomas Ulimwengu naye wanamtaja pia,” anasema.

UKIACHA SAMATTA NI DAIMOND PLATNUMZ

Anasema ukiachana na umarufu alionao Samatta, staa mwingine Mtanzania anayependwa na kutajwa nchini Congo ni mwanamuziki wa Bongofleva, Diamond Platnumz, wanayemuona anatikisa kwenye muziki Afrika.

“Wanapenda muziki wake na unapigwa sana, anazungumzwa kama mwanaharakati wa kupeperusha vyema bendera ya Tanzania dhidi ya nchi nyingine,” anasema.

ALIKOSA PESA ZA KWENDA CHUO

Ambokile amemaliza kidato cha sita mwaka 2016 katika Shule ya Sekondari ya Ivumwe iliyopo mkoani Mbeya, ndoto yake ilikuwa kusomea sheria lakini baada ya kukosa pesa za kujiunga na chuo akaamua kujikita kwenye soka.

Kidato cha nne alimaliza Shule ya Sekondari ya Meta iliyopo mkoani Mbeya ambapo alipata daraja la tatu, “Nimesoma na nina ndoto za kwenda chuo, nataka niwe mchezaji mwenye elimu yake, soka ni kazi ya heshima,” anasema.

“Ndoto zangu za kuwa mwanasheria zipo palepale, nategemea kuomba ambapo nitakuwa nasoma kwa njia ya mtandao, ilimradi tu nitimize kile nilichokuwa natamani tangu mdogo,” anasema.

KILICHOMUUMIZA MOYO

Anasema mambo mengi yalianza kwenda kombo baada ya mama yake mzazi kufariki mwaka 2013 kwani ndiye alikuwa akimsimamia kwenye shule na soka.

“Nilikosa sapoti, maisha yetu yakabadilika, kuna wakati nilikuwa natembea kwa mguu kwa umbali mrefu kwenda mazoezini wakati nachezea timu ya Ihefu kipindi hicho ilikuwa Ligi Daraja la Pili na makao makuu yake yalikuwa Mbalizi, nilijipa moyo kwamba nitashinda,” anasema.

JE SOKA LIMEMLIPA?

Anasema japokuwa hajafikia kilele cha ndoto zake lakini kiasi anashukuru kwa sababu anaweza kuitunza familia yake tofauti na mwanzo alipokuwa anatembea kwa miguu.

“Naona unafuu wa maisha tofauti na mwanzo ambapo nilikuwa naiona taswira yangu katikati ya miiba, nategemewa na ninaweza kumudu baadhi ya vitu,” anasema.

VIPI KUHUSU MAPENZI

Ambokile anasema sio mtu wa wanawake sana, hivyo hajui kitu kinachoitwa raha ama maumivu ya mapenzi. Anachokipa kipaumbele na kuandaa maisha yake kuwa na nguvu ya kiuchumi: “Starehe yangu nikiwa nyumbani ni kukaa na familia,” anasema.