Amekosea wapi Gaucho? ona sasa anaozea jela...

Muktasari:

Chenga na maudhi, ufundi, mbwembwe na pasi za bila kuangalia zilimfanya awe mfalme pale Nou Camp katika kipindi cha miaka mitano.

ASUNCION,PARAGUAY. Ukiyaangalia maisha ya sasa kisha ukarudi kutazama mambo ambayo miguu yake iliyafanya akiwa uwanjani, basi machozi yanaweza kukutoka na kujiuliza Ronaldinho Gaucho amekosea wapi? Inasikitisha sana!

Katika ubora wake aliufanya mpira uonekane mchezo rahisi, hakuna beki au mchezaji yeyote aliyetamani kuwa naye timu tofauti kwa sababu mwisho wa siku angeishia kumdhalilisha kwa chenga za maudhi.

Ronaldinho, 39, ndiye mchezaji mwenye kipaji kuwahi kucheza mpira, ndiyo maana katika ubora wake alishinda tuzo mbili za Mchezaji Bora wa Dunia wa Fifa, pamoja na Ballon d’Or mbili pia.

Chenga na maudhi, ufundi, mbwembwe na pasi za bila kuangalia zilimfanya awe mfalme pale Nou Camp katika kipindi cha miaka mitano.

Lakini, tangu astaafu rasmi soka mwaka 2018, mambo yamekuwa si mambo kwake, amehama kutoka kuwa mfalme ambaye kila aliloligusa alipokuwa uwanjani liligeuka dhahabu, hadi kuwa mtu wa majanga kila kukicha. Hii ni baadhi tu ya misala ambayo yamekuwa yakizidi kumpoteza.

Wanawake wawili

Mafanikio na pesa kwa miaka mingi yamemfanya kuwa asali wa warembo, lakini mwaka 2018 aliingia kwenye majanga ya kutaka kuwaoa wanawake wawili kwa wakati mmoja kitu ambacho mwenyewe alikanusha.

Iliripotiwa Ronaldinho alikuwa kwenye mchakato wa kutaka kuoa wapenzi wake wote wawili kwa mpigo kitu ambacho ni kosa kisheria Brazil.

Inaelezwa Gaucho alikuwa kwenye uhusiano na warembo wawili kwa wakati mmoja, Beatriz Souza na Priscilla Coelho na wote aliwavalisha pete na alikuwa anataka kuwaoa kwa wakati mmoja katika hafla ambayo ilipangwa kufanyika katika jumba lake la Pauni 5 milioni jijini Rio de Janiero.

Kitendo hicho ni kosa kisheria Brazil na adhabu yake ni kifungo cha miaka sita jela, lakini alifanikiwa kuukwepa msala huo kwa kukanusha taarifa hizo.

Kutengana

Mara baada ya siri hiyo kuibuka, Ronaldinho aliachana na Priscilla baada ya miaka sita, huku mwanamke huyo akipeleka kesi mahakamani akitaka kugawana mali na staa huyo zenye thamani ya Pauni 70 milioni.

Mama wa Priscilla, Maria Aldenice dos Santos aliibuka na kueleza jinsi ambavyo mwanawe pamoja na Beatriz walivyokuwa wanatoka kimapenzi na Ronaldinho kwa wakati mmoja.

“Alikuwa na chumba kimoja kwa ajili yake (Ronaldinho) na Priscilla, kisha chumba kingine kwa ajili yake na Beatriz,” alisema Maria.

“Walikuwa hawalali kitanda kimoja wote watatu, siku moja alilala (Ronaldinho) na Priscilla, nyingine alilala na Beatriz. Alikuwa anawapa wote wawili pesa sawa ya matumizi kila mwezi, na alikuwa anawapa zawadi zinazofanana, kuna wakati aliwahi kuwanunulia saa aina ya Rolex wote wawili.”

Maria anadai Priscilla alichoka maisha hayo mwishoni mwa mwaka 2018 na akaachana na Ronaldinho baada ya ugomvi mkubwa.

Maria alisema: “Aliniambia Ronaldo (Ronaldinho) alianza kwenda kujirusha peke yake na kumuacha (Priscilla) nyumbani peke yake. Kisha akaona meseji za wanawake wengine kwenye simu yake, Beatriz hakuwepo nyumbani alienda London kula Krismasi. “Aliamua kumuhoji kuhusu hizo meseji, lakini hakutaka kuzungumza. Aliingia (Ronaldinho) kwenye gari lake na Priscilla alimfuata akimtaka wazungumze lakini akagoma. Ndiyo maana akaamua kuachana naye.”

Vitu vyataifishwa

Mwaka 2018, wakati akipitia kipindi kigumu kifedha, Mwendesha mashtaka wa Brazil na polisi walivamia nyumbani kwake na kutaifisha baadhi ya mali zake, yakiwemo magari ya kifahari na michoro ya pesa ndefu. Mwezi mmoja kabla ya kuvamiwa na polisi, hati yake ya kusafiria ilitaifishwa na ikagundulika kuwa alikuwa na Pauni 5 milioni tu kwenye akaunti yake na hakuwa na uwezo wa kulipa deni lililotokana na mfuko wake wa kijamii.

Maafisa kutoka ofisi ya mwendesha mashtaka walichuku magari yake mawili aina ya BMW na Mercedes-Benz, walifanya hivyo ili kuzalisha pesa za faini ambazo alitakiwa kulipa.

Mchoro uliochorwa na msanii Andre Berardo ulichukuliwa kutoka katika nyumba inayomilikiwa na familia ya Ronaldinho jijini Porto Alegre.

Kwa mujibu wa Wizara ya Umma ya Brazil, taasisi inayomilikiwa na staa huyo pamoja na kaka yake, Assis Moreira, ikisaidia watoto wanaishi kwenye maisha magumu ilikutwa na hatia ya kufanya uharibifu wa mazingira.

Walidaiwa kukata misitu na kujenga kwenye chanzo cha maji bila leseni, hivyo walitakiwa kulipa faini ya Pauni 1.75 milioni.

Mijengo 57 yataifishwa

Kiangazi mwaka jana, mijengo 57 ya Ronaldinho ilitaifishwa na serikali na hati yake ya kusafiria ya Brazil na ile ya Hispania zote zilitaifishwa. Deni lake la uharibifu wa mazingira halikuwa limelipwa na lilikuwa kufikia Pauni 2 milioni. Huku kukiwa na taarifa kuwa alikuwa na deni lingine la Pauni 1.69, lakini taarifa hizo hazikuthibitishwa na mahakama kutokana na sheria ya usiri wa mtuhumiwa, huku wakili wake naye akigoma kuzungumzia suala hilo.

Jela inamuita Paraguay

Wakati akiwa na kesi kibao Brazil, Ronaldinho amejikuta kwenye majanga, safari hii nje ya taifa lake, hii ni baada ya kuingia Paraguay kwa kutumia hati ya kugushi ya kusafiria. Msala huo ulisababishwa juzi kati avamiwe hotelini kwake na kuhojiwa kwa masaa nane na mwendesha mashtaka wa Paraguay akituhumiwa kuingia kwenye nchi hiyo kwa kutumia hati ya kusafiria iliyochakachuliwa.