Arsenal, Man City kikaangoni

Tuesday March 17 2015

Manchester, England. England inaweza kukosa mwakilishi kwa mara ya pili ndani ya miaka mitatu katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kama Arsenal na Manchester City watashindwa kulipa kisasi katika michezo yao ya leo na kesho.

Arsenal ilikubali kichapo cha mabao 3-1 nyumbani dhidi ya Monaco na sasa inakutana na miamba hiyo nchini Ufaransa, wakati City ikitakiwa kugeuza kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Barcelona ili kutinga katika robo fainali ya mashindano hayo kwa mara ya kwanza.

Ni kazi ngumu kwa miamba hiyo ya England, lakini inaweza kuchukua ari ya Schalke na Paris Saint-Germain waliopambana ugenini wiki iliyopita.

Mabingwa watetezi, Real Madrid waliichapa Schalke 2-0 nchini Ujerumani, lakini hali ilikuwa mbaya nyumbani kwani waliitoa timu hiyo kwa mabao 5-4, wakati PSG wakicheza 10 uwanjani dhidi ya Chelsea tangu dakika ya 31, lakini walilazimisha sare na kusonga mbele kwa mabao ya ugenini walipopata matokeo ya 2-2 Stamford Bridge.

Mechi nyingine wiki hii zinaonekana kuwa katika uzani sawa. Bayer Leverkusen wataivaa Atletico wakiwa wameifunga Madrid 1-0 nchini Ujerumani na Juventus wataulinda ushindi wao wa 2-1 dhidi ya Borussia Dortmund.

Arsenal wanaonekana kuwa na mabadiliko wanapojiandaa kuivaa Monaco kutokana na kufanya vizuri katika mchezo wao uliopita wa Ligi Kuu England.

Ushindi dhidi ya Everton, QPR na West Ham katika ligi na ule dhidi ya Manchester United katika Kombe la FAumeufanya msimu wa Arsenal kuwa mzuri na wanatakiwa kuwa na kasi hiyo katika Uwanja wa Louis II.

Safu ya ulinzi ya Monaco imeonekana kuwa ngumu msimu huu ikiwa imeruhusu mabao 20 katika michezo 28 ya Ligi Kuu Ufaransa, lakini pia wameonyesha ukomavu kwa kufungwa na PSG na Bordeaux pekee.

Lakini pia, Arsenal haijawahi kupoteza mchezo nchini Ufaransa ikiwa na rekodi nzuri na timu za nchi hiyo katika michezo ya marudiano.

 Hata hivyo, Kocha wa Monaco, Leonardo Jardim amekuwa na matumizi mazuri ya mashambulizi ya kushitukiza yaliyomsaidia katika mchezo wa kwanza dhidi ya Arsenal.

Licha ya Lionel Messi kukosa penalti katika mchezo wa kwanza, Man City wanatakiwa kuwa makini na kikosi hicho watakapokuwa katika Uwanja wa Camp Nou kesho.

LIGI YA MABINGWA ULAYA

Leo, Jumanne

A.Madrid             v              B.Leverkusen (Saa 4:45 usiku)   

Monaco               v              Arsenal (Saa 4:45 usiku)

Kesho, Jumatano

B.Dortmund       v Juventus          (Saa 4:45 usiku)

Barcelona            v Man City           (Saa 4:45 usiku)

Advertisement