Hivi hapa vipimo vya Samatta Aston Villa vitakazomjenga au kumbomoa

Muktasari:

  • Msimu uliopita alifunga mabao 20 katika mechi 28 kwenye Ligi ya Ubelgiji na kuwa kinara wa mabao, huku akiuweka wavuni mara sita kwenye mechi 12 alizocheza kwenye Europa League.

LONDON, ENGLAND. UKANDA wa Afrika Mashariki umeibuka kwenye shangwe kubwa baada ya supastaa na nahodha wa Tanzania, Mbwana Samatta kukamilisha uhamisho wake wa kutoka KRC Genk na kwenda kutua Aston Villa ya Ligi Kuu England.

Jumanne iliyopita, Aston Villa yenye maskani yake Villa Park ilitoa taarifa ya kuinasa rasmi saini ya Samatta kwa kumsainisha mkataba wa miaka minne na nusu, huku jambo hilo likimfanya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kujiunga na timu ya Ligi Kuu England, akifuata nyayo za nahodha wa Kenya, Victor Wanyama.

Samatta, ambaye aliwahi kuzitumia Simba na TP Mazembe msimu huu amefunga mabao saba katika mechi 20 alizocheza kwenye Ligi Kuu Ubelgiji (Jupiler League). Amefunga pia mabao matatu katika mechi sita alizocheza hatua ya makundi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ikiwamo kwenye mechi ya kipigo cha mabao 2-1 ilichokipata Genk kutoka kwa Liverpool, Novemba mwaka jana.

Msimu uliopita alifunga mabao 20 katika mechi 28 kwenye Ligi ya Ubelgiji na kuwa kinara wa mabao, huku akiuweka wavuni mara sita kwenye mechi 12 alizocheza kwenye Europa League.

Hivyo, kwenye suala la kufunga, Samatta hajawahi kuwa na tatizo na sasa mashabiki wanasubiri kuona atakachokifanya katika mechi yake ya kwanza akiwa na Aston Villa na mengi nyingine zitakazofuata baada ya hapo. Kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, Aston Villa ipo pointi mbili tu juu ya shimo la kushuka daraja, hivyo itahitaji huduma bora kwa mastaa wake akiwamo Samatta ili kupambana kujinasua kwenye hatari hiyo ya kuporomoka kwenye Championship.

Hizi hapa mechi 10 za mwanzo zitakazomjenga au kumbomoa Samatta katika maisha yake huko Villa Park.

Leicester City- Villa Park

Staa Samatta mechi yake ya kwanza akiwa na jezi za Aston Villa inatarajia kuwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Villa Park, wakati chama lake hilo litakaporudiana na Leicester City kwenye nusu fainali ya Kombe la Ligi. Mechi ya kwanza iliyopigwa King Power ilimalizika kwa sare ya 1-1, hivyo Jumanne, Januari 28 itapigwa mechi ya marudiano huku Samatta akitarajia kucheza mechi yake ya kwanza ambapo atakuwa na shughuli ya kukabwa na mabeki wenye uzoefu wa soka la England kama vile Jonny Evans.

Bournemouth- Dean Court

Wakati mashabiki wa soka kwa nchi za Afrika Mashariki wakisubiri kumwona Samatta akicheza mechi yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu England, hilo linaweza kutimia kwa mchezo wa ugenini huko Dean Court atakapokwenda kuwavaa Bournemouth, Februari Mosi. Mechi hiyo itafungua mwanzo wa Samatta na maisha yake kwenye Ligi Kuu England na wengi wanasubiri kama ataweza kuwa mwiba mchungu kwa mabeki wa Bournemouth katika mchakamchaka huko wa kupambana timu isishuke daraja.

Tottenham- Villa Park

Mchezo wa pili huu wa Ligi Kuu England anaoweza kucheza Samatta kwenye ligi hiyo. Mechi hii itapigwa Februari 16, ambapo Aston Villa itakuwa kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Villa Park kulikaribisha jeshi la Jose Mourinho, Tottenham Hotspur. Kwenye mchezo huo, Samatta atakuwa na wakati mgumu wa kukabiliana na Mourinho na staili yake ya kuweka mabeki wengi, huku moja kwa moja akiwa ya shughuli na kukumbana na mabeki wagumu kama Jan Vertonghen na wenzake. Hata hivyo, siku za karibuni beki ya Spurs imekuwa na matatizo makubwa, hivyo Samatta anaweza kutikisa nyavu katika mchezo huo.

Southampton- St Mary’s

Gari la Southampton kwa sasa linaonekana limewaka na hakika mechi hii itakuwa ngumu kwa Aston Villa katika jitihada zao za kuhakikisha wanashinda ili kuondoka kwenye hatari ya kushuka daraja. Bila ya shaka kupata matokeo kwenye mchezo huo, Aston Villa itahitaji huduma muhimu kabisa kutoka kwa straika wao mpya katika kuwafungia mabao, huku mchezo huo wa Southampton ukiwa wa tatu kwa straika huyo wa Taifa Stars huko kwenye Ligi Kuu England. Hado hapo atakuwa na dakika 270 kwenye ligi hiyo zitakazotoa taswira ya kile anachoweza kukifanya.

Sheffield United - Villa Park

Baada ya kumalizana na wagumu Southampton, Samatta atakuwa na mtihani mwingine wa kuiongoza timu yake mbele ya wagumu wengine, Sheffield United. Uzuri wa mechi hii itapigwa Villa Park, ambapo utakuwa mchezo wake wa tatu wa kwa Samatta kucheza katika uwanja wa nyumbani Villa Park, lakini ukiwa mchezo wa pili wa Ligi Kuu England kucheza uwanjani hapo. Makali yake ndicho kitu kitakachowafanya mashabiki wa Villa Park kumkubali kama atahakikisha anawapigia mabao kama ambavyo alikuwa akifanya huko Genk.

Leicester City- King Power

Kama Samatta atakuwa amepata bahati ya kucheza kwenye nusu fainali ya pili ya Kombe la Ligi dhidi ya Leicester City na kisha akapangwa Machi 7 huko King Power, basi atakuwa amecheza na wakali hao wao wanaonolewa na Brendan Rodgers mara mbili huku safari hii ikiwa ni mchezo wa Ligi Kuu England. Kwenye mchezo huo, Samatta atataka kumwonyesha Jamie Vardy uwezo wake wa kufunga mabao huku itakuwa na heshima kubwa kwake kama ataweza kutikisa nyavu kwenye uwanja huo wa King Power.

Chelsea - Villa Park

Baada ya kumalizana na Leicester City kwenye ligi, Samatta atakuwa na mtihani mwingine wa kuhakikisha anaisaidia Aston Villa yake kwenye mchezo mgumu kabisa dhidi ya Chelsea. Mechi hiyo itakayopigwa uwanjani Villa Park itakuwa Machi 14, huku staa Samatta akiwa na kazi ya kukabiliana mabeki wagumu kama Antonio Rudiger katika mchezo huo. Kuwakabili Chelsea itakuwa na umuhimu mkubwa kwa Samatta kwa sababu ni moja ya mechi ambazo mashabiki wake wa Afrika Mashariki na kwingineko duniani watahitaji kuona kitu gani atakachofanya kwenye mchezo huo.

Newcastle United - St James’ Park

Machi 21, Aston Villa itasafiri hadi jijini Newcastle kwenda kumenyana na wenyeji wake Newcastle United katika mchezo wa Ligi Kuu England. Kwa kipindi hicho joto litakuwa kubwa la mapambano ya kukwepa kushuka daraja, hivyo straika Samatta atakuwa kwenye wakati mgumu wa kuhakikisha kwamba chama lake linafanya kweli ugenini na kupata matokeo yatakayowafanya waendelee kubaki kwenye ligi kwa msimu mwingine. Aston Villa wamerejea Ligi Kuu England msimu huu, hivyo watahitaji kupambana kuendelea kubaki huku Samatta akiwa na jukumu moja kubwa la kuhakikisha wababe hao wanabaki.

Wolves - Villa Park

Wolves haijawahi kuwa timu nyepesi kabisa kutokana na wachezaji waliopo kwenye kikosi chao kuwa na uzoefu na vipaji vikubwa. Kitu kizuri ni kwamba mchezo huo utakaopigwa Aprili 4, Samatta na jeshi lake watakuwa nyumbani Villa Park kuwakabili wakali Wolves, ambao mara nyingi wamekuwa na mambo magumu ndani ya uwanja unapokabiliana nao. Mechi hiyo itakuwa na taswira halisi ya mwenendo wa msimu wa Aston Villa kwenye Ligi Kuu England msimu huu huku wakihitaji ushindi pengine katika kila mechi kutoka sasa ili kuhakikisha wanaendelea kutamba kwenye ligi.

Liverpool - Anfield

Mara ya mwisho, Samatta alipokwenda Anfield alipiga bao matata kabisa kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya alipowakabili wenyeji wa mahali hapo, Liverpool. Lakini, Aprili 11, atarudi kwenye uwanja huo akiwa na timu mpya, Aston Villa itakapokwenda kulikabili jeshi la Jurgen Klopp katika Ligi Kuu England. Uzuri wa mchezo huo ni kwamba unaweza kufanyika wakati Liverpool tayari ikiwa mabingwa wa ligi, lakini kama utakuwa tofauti basi unatazamiwa kuwa na upinzani mkali huku Samatta akitarajia kwenda kumpa wakati mgumu tena beki bora duniani, Virgil van Dijk mbele ya mashabiki wake.