VIDEO: Aussems: Mechi ya KMC ni mazoezi tu

SIMBA itapambana na KMC katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems amesema atatumia mchezo huo kuwaweka fiti wachezaji wake wakati huu wakijiandaa kuikabili Ruvu Shooting kwenye Ligi Kuu Novemba 23.

Aussems alisema mchezo huo utawasaidia wachezaji wake waliopo na timu hiyo kujua  mapungufu yao ili kuyarekebisha kabla ya ligi kuendelea.

"Wachezaji wangu 10 wako katika majukumu ya timu za Taifa hivyo hawa waliobaki tukaona tuwatafutie mechi ya kirafiki ili nao waendelee kuwa fiti.

"Naiita  ni mechi ya mazoezi na sio ya kirafiki hivyo itanisaidia kujua maeneo yapi  bado kuna shida ili kurekebisha kabla hatujarejea kwenye mechi ya ligi" alisema Aussems.

Katika mazoezi hayo wachezaji wote walihudhuria kasoro 10 walio katika timu zao za Taifa huku John Bocco pekee akifanyishwa mazoezi ya peke yake.