Aussems: Simba kuna viongozi waongo, vilaza

Wednesday December 4 2019

 

By Eliya Solomon

Dar es Salaam. Aliyekuwa kocha wa Simba SC, Patrick Aussems 'Uchebe' amesema ili klabu hiyo, iendelee inatakiwa kuachana na viongozi waongo na wasiokuwa na uelewa katika bodi yake ya wakurugenzi.

Aussems alisema hayo jana kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter ambao aliutumia kuwaaga mashabiki na wachezaji wa Simba kufuatia kuondoka kwake nchini baada ya kumalizana na klabu hiyo.

Kocha huyo, Mbelgiji aliposti ujumbe huo, uliokuwa ukisomeka, "Asanteni mashabiki wa Simba. Nawatakia kila la kheri. Ili Simba ikue, lazima watimue waongo na watu wasio na elimu kwenye bodi ya wakurugenzi."

Ujumbe huo, uliendelea kwa kusomeka kuwa sasa ni muda wa kufurahia na familia yake huku akimalizia, "Kwaheri Tanzania."  Kocha ameondoka akiicha Simba ikiwa katika kilele cha msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Moja ya mambo yaliyopelekea Aussems awe kipenzi cha mashabiki wa Simba ni kitendo cha timu hiyo kutamba katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita wa 2018/2019.

Huku ikiwa inashiriki kwa mara ya kwanza baada ya kukosa mashindano kwa takribani miaka mitano, Simba ikiwa chini ya Aussems iliweza kutinga hatua ya robo fainali ya mashindano hayo ambapo ilitolewa kwa kipigo cha jumla cha mabao 4-1 na TP Mazembe ya DR Congo.

Advertisement

Ilianza kwa kuitoa Mbabane Swallows ya Swaziland kwa ushindi wa jumla wa mabao 8-1 na katika hatua ya kwanza wakaitupa nje Nkana FC ya Zambia kwa kuichapa jumla ya mabao 3-2 kisha wakatinga hatua ya makundi ambapo waliangukia katika Kundi D lililokuwa na timu za Al Ahly, AS Vita Club na JS Saoura.

Katika hatua hiyo ya makundi walimaliza wakiwa nafasi ya pili nyuma ya Al Ahly wakikusanya pointi tisa baada ya kupata ushindi katika mechi tatu na kupoteza tatu kabla ya kukwaa kigingi mbele ya Mazembe katika robo fainali.

Hata hivyo baada ya kutamba msimun uliopita, mambo hayakuwa mazuri kwa Aussems msimu huu kwani walijikuta wakiondoshwa mapema na UD Songo ya Msumbiji katika raundi ya awali kwa sheria ya bao la ugenini.

Timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana huko Msumbiji na katika mchezo wa marudiano hapa nchini zilifungana bao 1-1.

Kiujumla chini ya Aussems, Simba imecheza jumla ya michezo 14 ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imepata ushindi katika mechi sita, imetoka sare mitatu na imepoteza mechi tano, huku ikiwa imefunga mabao 20 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 22.

Advertisement