Aussems: Tunazitaka pointi tatu za AS Vita

Saturday January 19 2019

By Khatimu Naheka, Mwananchi

Kinshasa. Simba inashuka uwanjani leo kucheza mchezo wake wa pili ugenini dhidi ya AS Vita Club na kocha wake, Patrick Aussems akisema wataingia kusaka pointi tatu na sio kupaki basi.

Simba inaingia katika mchezo huo wa pili ikiwa na pointi tatu baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JS Soura ya Algeria wiki iliyopita.
Wanakutana na AS Vita iliyopokea kipigo cha mabao 2-0 ugenini nchini Misri dhidi ya Al Ahly na kufanya Simba kuongoza kundi lao D Ligi ya Mabingwa Afrika wakifuatiwa na Ahly. AS Vita ni ya tatu na JS Saoura ni ya mwisho.
Kikosi kamili cha Simba kilichoondoa nchini Alhamisi asubuhi kilitua salama nchini DR Congo jijini Kinshansa majira ya saa 1:35 mchana bila kupata usumbufu wowote.
Salama ya Simba ilikuwa ni kuwatanguliza watu watatu DR Congo ambao walifanya kazi ikiwemo maandalizi na mambo ya muhimu kwa timu.
Wakiongozwa na Mjumbe wa Bodi ya Simba, Mulamu Ng’ambi akisaidiana na Mratibu wa timu hiyo, Abbas Ally tayari walishatafuta usafiri na hoteli kwa ajili ya timu yao.
Kikosi hicho kimeweka kambi katika hoteli ya Venus ambayo haipo mbali na katikati ya mji.
Hoteli hiyo ya Simba pia hutumiwa na wapinzanj wa Vita ambao ni Club DC Motema Pembe.

Juzi Simba ilifanya mazoezi yake ya kwanza mara baada ya kuwasili yakifanyika katika uwanja wa mashujaa ambao ndiyo uwanja utakaotumika kwenye mechi ya leo.
Uwanja huo unaochukua mashabiki 75,000 unatumia nyasi za bandia lakini kocha wa Simba Patrick Aussems alisema tayari walikwisha kujiandaa na hilo kwa kuweka kambi Kisiwani Zanzibar na kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Amaan.
Jana jioni Simba ilifanya mazoezi ya mwisho na yalifanyika kwa kiwango bora huku wachezaji wakionekana kuwa na morali kubwa.
Katika mazoezi hayo Aussems alionekana kutotaka timu kupaki basi na kutaka kushambulia mwanzo mwisho.
Alichofanya Aussems ni kuongeza uimara katika safu yake ya kiungo akijaribu kuanza na viungo wawili wakabaji na wawili washambuliaji.
Aussems alionekana akijiandaa kuwatumia Jonas Mkude, James Kotei lakini pia akipanga kuwatumia Hassan Dilunga na Clatous Chama katika viungo vya juu.
Katika safu ya ushambuliaji hakuna shaka raia huyo wa Ubelgiji atakuwa na akili ya kuwatumia Emmanuel Okwi na Meddie Kagere ambao wamekuwa katika ushirikiano mkubwa wanapocheza pamoja.
Katika mechi iliyopita Okwi alimtengenezea bao moja Kagere huku lingine likitengenezwa na Chama.
Katika ulinzi Aussems alionekana kutofanya mabadiliko akipanga kuanza na Nicholas Gyan, nahodha Mohammed Hussein, Juuko Murushid na Pascal Wawa.
Akizungumza jana Aussems alisema wanatambua kwamba watakuwa na mchezo mgumu lakini wamekuja kutafuta matokeo.
Aussems alisema anatambua AS Vita wanahitaji matokeo baada ya kupoteza mchezo wa kwanza na wanaiheshimu lakini hawakuja kujilinda nao watatafuta matokeo.
“Tunatambua Vita Club ni timu ngumu na itahitaji kutafuta matokeo baada ya kupoteza mechi ya kwanza na kwa kuwa wanacheza nyumbani presha itakuwa kwao,” alisema Aussems.
“Tumejiandaa vyema kama Simba na malengo yetu hapa ni kutafuta matokeo hatujaja kujilinda tumekuja kutafuta matokeo.”
Mchezo huo utaanza saa 1:00 usiku kwa saa za Tanzania huku kwa Congo itakuwa ni saa 11 jioni.

Advertisement