Aussems abebeshwa zigo dirisha dogo

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wameanza mapema harakati za kukiimarisha kikosi chao kwenye dirisha dogo la usajili linalotarajiwa kufunguliwa Novemba 15 hadi Desemba 15.

Mipango ya mabosi na benchi la ufundi la Simba ni kuongeza mshambuliaji na kiungo kwa ajili ya kuimarisha idara hizo mbili.

Habari za ndani ambazo Mwanaspoti limezinasa ni kwamba, ofisa mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Senzo Mazingisa amempa mamlaka kocha Patrick Aussems kutafuta washambuliaji watatu wenye uwezo mkubwa kisha watafanya uamuzi wa kubaki na mmoja. “Tumepanga kuongeza mshambuliaji katika dirisha dogo kutokana John Bocco kuwa na majeraha ya mara kwa mara, hivyo mwalimu kulazimika kumtumia Meddie Kagere pekee,” alisema mmoja wa viongozi wa juu wa timu hiyo.

“Aussems amepewa nafasi hiyo ya kuleta taarifa za washambuliaji watatu na mwenye kiwango cha juu ndiye tutabaki naye. Tunaangalia kwenye dirisha hili uwezekano wa kuwapata hawa jamaa hata ikiwa ni kwa mkopo.

“Kama tukimpata mshambuliaji wa kigeni sioni nafasi ya Wilker Da Silva kuendelea kubaki, lakini kuhusu taarifa za Jesse Were wa Zesco United, ambaye mkataba wake unamalizika huyo jina lake lililetwa na wakala wake hapa Simba, lakini tulimkataa sababu ya umri.”

Kwa upande wake, Aussems alisema kwa sasa hawezi kueleza kama anaweza kuongeza mchezaji mwingine kutokana na baadhi waliosajiliwa kutocheza mpaka sasa.

“Mahitaji ya mshambuliaji ni kweli yapo kutokana na matatizo ya majeruhi ya mara kwa mara jambo ambalo muda mwingi Kagere hutumika peke yake.

“Lakini, bado tunaendelea kuangalia kwenye maeneo mengine na kama atapatikana mtu sahihi basi kulingana na mahitaji yetu tutamsajili hata kama kwenye dirisha dogo la usajili,” alisema.

Aliyekuwa ofisa mtendaji mkuu wa Simba, Crescentius Magori alisema kama angepata nafasi ya kushauri katika uongozi wa timu wafanye usajili wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao wakati huu kutokana kipindi cha dirisha kubwa wachezaji wengi kuwa ghali. “Nikiangalia timu ilivyo sioni nafasi kubwa ya usajili kwa wakati huu wa dirisha dogo, kwa maana mahitaji ya kuongeza nguvu labda msimu ujao katika mashindano ya kimataifa, lakini kwa timu za hapa ndani Simba inaweza kuonyesha ushindani kwa timu yoyote,” alisema.

“Nadhani hata hayo mahitaji ya mshambuliaji ni kutokana na majeraha ya Bocco na kutokuwa fiti kwa Da Silva na kama wote wanakuwa sawa, wakishirikiana na Kagere watakuwa wamezidi kuimarika.”