Aveva, Kaburu waandika barua kwa DPP

Friday October 11 2019

 

By TAUSI ALLY

WAKILI wa Serikali Wankyo Simon ameieleza Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa aliyekuwa rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na Makamu wake Godfrey Nyange 'Kaburu'  wameandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Imeelezwa barua hiyo ni kwa ajili ya kutaka kuanza majadiliano ya namna ya kuimaliza kesi hiyo inayowakabili.
Hata hivyo, Wankyo Oktoba 11 aliiambia Mahakama kuwa washtakiwa wote wapo na kesi iliyopangwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi kuhusiana na hoja mbalimbali zilizowasilishwa na upande wa mashtaka kuhusu mahakama kuwaondolea mashtaka ya utakatishaji.
Baada ya kuelezwa hayo, Hakimu Simba alisema bado hajamaliza kuandaa hivyo aliiahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 18, mwaka huu ambapo atatoa uamuzi.
Hatua hiyo ilifikiwa na upande wa mashtaka baada ya mahakama kuwaondolea mashtaka mawili ya utakatishaji,  kati ya 10 yaliyokuwa yakiwakabili Aveva na  Kaburu kwani upande wa mashtaka ilielezwa walishindwa kuthibitisha mashitaka hayo.
Hata hivyo, washtakiwa hao pamoja na mwenzao Zacharias Hansppope walikutwa na kesi ya kujibu katika mashtaka saba ambayo ni kughushi, kula njama, matumizi mabaya ya madaraka, kutoa nyaraka za uongo na kutoa maelezo ya uongo ambayo upande wa mashitaka umeweza kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa.
Kufuatia kuondolewa kwa shitaka la utakatishaji  washtakiwa wamepatiwa masharti ya dhamana kwasababu mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo yaliwanyima dhamana hayapo.
Kwa mujibu wa uamuzi huo umetolewa na Hakimu Simba alisema ni jukumu la upande wa mashitaka kuthibitisha mashitaka yote kwa washitakiwa na kila shitaka linatakiwa kuthibitishwa pekee yake na sio kwa kutegemeana.
Baada ya kuchambua ushahidi wa mashahidi 10 wa upande wa mashitaka, ukiacha shitaka la tano na sita mahakama iliona kuwa washitakiwa wana kesi ya kujibu katika shitaka la 1, 2, 3, 4, 7, 8 na 9  isipokuwa shitaka la tano na sita  ambayo ni ya  utakatishaji yaliyoondolewa.
Kufuatia kuondolewa kwa mashtaka hayo, Wakili wa washtakiwa hao Nehemia Nkoko aliiomba mahakama kuwapatia wateja wake dhamana kwani mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo yaliyokuwa yanawanyima dhamana hayapo.
Wakili wa Takukuru, Leornad Swai alipoulizwa kama ana pingamizi lolote juu ya dhamana alidai hawana pingamizi.
Hakimu Simba aliwapatia masharti ya dhamana washtakiwa ya kuwa na wadhamini  waili watakaosaini bondi ya Sh 30 Milioni  kwa kila mmoja pamoja na kuwa na vitambulisho
Katika shtaka la kwanza,  Aveva na Kaburu wanadaiwa kula njama ya kutenda kosa la matumizi mabaya ya madaraka.
Katika shtaka la pili la Aveva na Kaburu wanadaiwa kutumia vibaya madaraka yao kwa kuandaa fomu ya kuhamisha fedha Dola za Kimarekani 300,000 kutoka kwenye akaunti ya Simba iliyoko benki ya CRDB Azikiwe kwenda kwenye akaunti binafsi ya Aveva iliyoko benki ya Barclays.
Katika shtaka la tatu, Aveva na Kaburu  wanadaiwa kwa pamoja kughushi nyaraka iliyokuwa ikionesha Simba inalipa mkopo wa USD 300,000 kwa Aveva kitu ambacho sio kweli.
Katika shtaka la nne Aveva anadaiwa katika banki ya CRDB anadaiwa kutoa nyaraka ya uongo ikionesha Simba wanalipa mkopo wa USD 300,000
Aveva anadaiwa kuwa katika Benki ya Baclays Mikocheni alijipatia USD 187,817 wakati akijua zimetokana na kughushi.
Katika shtaka la sita, Kaburu anadaiwa kumsaidia Aveva kujipatia USD 187,817 kutoka kwenye akaunti ya Simba wakiwa wanajua fedha hizo zimetokana na zao la kughushi.
Aveva, Kaburu na Hans Poppe  wanadaiwa kughushi hati ya malipo ya kibiashara wakionesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zina thamani ya USD 40,577 huku wakijua kwamba siyo kweli
Katika shtaka la nane, Aveva anadaiwa kuwasilisha hati ya malipo ya kibiashara ya uongo  kwa Levison Kasulwa  kwa madhumuni ya kuonesha kwamba Simba wamenunua nyasi bandia zenye thamani ya USD 40,577
Shtaka la tisa, Aveva, Kaburu na Hanspope wanadaiwa kuwasilisha nyaraka za uongo kuonesha kuwa Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya USD 40,577.

Advertisement