Azam, Simba hesabu tupu

Dar es Salaam. Hatima na hesabu za Azam FC katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ipo mikononi mwa Simba wakati timu hizo zitakapovaana leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi 50, Azam inalazimika kuibuka na ushindi dhidi ya Simba ili kuendelea kubaki kwenye mbio za ubingwa vinginevyo ndoto za kurudia kile ilichofanya msimu 2013/2014 kwa kutwaa ubingwa haziwezi kutimia.

Ushindi dhidi ya Simba si tu utaifanya ipunguze pengo la pointi baina yake na vinara wa ligi Yanga kubaki nane, pia utaisaidia kuwa juu ya Simba inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 42 kwa kuwa itafikisha pointi 52.

Azam ikishinda na Simba ikapata ushindi katika mechi saba za viporo zitakazobaki ili wawe na idadi sawa ya mechi dhidi ya Azam na Yanga, Simba itakuwa mbele ya Azam kwa pointi 13.

Endapo Azam itapoteza, Simba itafikisha pointi 45 na endapo baadaye itacheza viporo vyao na kupata ushindi na kisha kuwa idadi sawa ya michezo, Simba itakuwa mbele ya Azam kwa tofauti ya pointi 16.

Namna pekee ya Azam kumpiku Simba ni kuombea ipoteze mechi saba kati ya 13 ambazo itakuwa imebakiza kabla ya ligi kumalizika jambo ambalo huenda likawa gumu kutokana na ubora wa Simba.

Ukiondoa suala la matokeo, Azam inaingia leo ikiwa na presha ya rekodi mbovu iliyokuwa nayo katika siku za hivi karibuni ambapo katika mechi nne mfululizo haijapata ushindi.

Timu hiyo ina pointi tatu katika mechi nne ikitoka sare mara tatu na kupoteza mchezo mmoja. Ilianza kutoka sare na Alliance ikalazimisha sare ya bao 1-1 na Lipuli, ilitandikwa 1-0 na Prisons na juzi ilitoka sare na Coastal Union.

Hofu kwa Azam ni safu ya ulinzi ambayo imeruhusu nyavu zao kutikiswa mara kwa mara na mfano ni mechi tano za hivi karibuni za ligi ambapo imefungwa mara tano jambo ambalo si zuri kuvutia kwa timu inayosaka ubingwa.

Wakati hali ikiwa hivyo kwa Azam, Simba ipo katika nyakati za neema ikijivunia muendelezo wa matokeo bora iliyopata katika mechi za mashindano katika siku za hivi karibuni.

Simba inacheza na Azam ikiwa imetoka kupata ushindi kwenye mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu dhidi ya Yanga na African Lyon, lakini kabla ya hapo ilikuwa imeifunga Al Ahly ya Misri bao 1-0 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Azam inapaswa kumchunga Meddie Kagere ambaye amekuwa mhimii wa Simba katika safu yake ya ushambuliaji ambayo ameifungia mabao tisa katika Ligi Kuu.

“Jambo la msingi ni kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu kwa dakika zote tisini, naamini kama tutatimiza hilo tutaibuka na ushindi,”alisema kocha wa Azam Hans van der Pluijm.

Kwa upande wa Simba, mchezaji wanayepaswa kumchunga zaidi ni kiungo mshambuliaji Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ambaye amekuwa ndiye chachu ya kuzalisha mabao ya timu hiyo msimu huu.

Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema anaamini timu yake itashinda kutokana na maandalizi mazuri wanayofanya ingawa anajua mechi itakuwa ngumu. “Azam FC ni timu kubwa na mechi haiwezi kuwa rahisi kwa upande wetu, lakini tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunakuwa na mwendelezo wa kupata matokeo mazuri,” alisema Aussems.