Azam FC yazifutia aibu Simba, Yanga Kombe la Mapinduzi

Muktasari:

  • Unaweza kusema ilikuwa mechi ya kisasi baada ya timu hiyo ya Uganda kuzifanyia roho mbaya Simba, Yanga na Azam FC yenyewe kwenye michezo ya awali kwa kuzitandika bila huruma, huku ikiiondoa Yanga kwa matuta kwenye hatua ya nusu fainali huku Simba wakiondolewa kwenye hatua ya makundi.

Dar es Salaam. Nahodha wa Azam FC, Himid Mao alidhihirisha mbele ya  umati uliokuwa kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar mwari ametua kwnye kikosi hicho cha Chamazi baada ya kupokea Kombe la Mapinduzi kwa kuichapa URA mikwaju ya penalti 4-3.

Unaweza kusema ilikuwa mechi ya kisasi baada ya timu hiyo ya Uganda kuzifanyia roho mbaya Simba, Yanga na Azam FC yenyewe kwenye michezo ya awali kwa kuzitandika bila huruma, huku ikiiondoa Yanga kwa matuta kwenye hatua ya nusu fainali huku Simba wakiondolewa kwenye hatua ya makundi.

Azam FC imefanikiwa kuondoa aibu ya timu za Ligi Kuu Tanzania Bara kutandikwa na URA kila ziliposogea kwenye anga zake.

Mchezo wa fainali wa jana Jumamosi ulishuhudiwa na Rais wa Zanzibar, Dk Ally Mohammed Shein ambaye pia ndiye alikuwa mgeni rasmi kwenye huku akiwakabidhi Kombe la ubingwa wa mapinduzi kikosi hicho cha Chamazi.

Mashindano hayo yamemalizika huku URA ikibaki kuwa gumzo baada ya kuonyesha kiwango kizuri kwenye mashindano hayo baada ya kuzifunga timu vigogo ziliopo Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye michezo yake ya awali, kabla ya kupoteza mchezo wa jana na kuipa nafasi Azam kutetea taji hilo la ubingwa.