Azam sasa yapunguzwa kasi Ligi Kuu

Dar es Salaam. Azam FC imeendeleza rekodi ya kutopata ushindi katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya jana kutoka sare ya bao 1-1 na Lipuli ya Iringa.

Azam ilikuwa ugenini katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Samora, mkoani Iringa.

Lipuli ambayo ilikuwa mwenyeji wa mchezo huo ilipata bao la kuongoza dakika ya 45 lililofungwa na Daruesh Saliboko.

Bao hilo lilidumu hadi dakika ya 80 kabla ya kiungo wa Azam, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kufunga bao la kusawazisha.

Azam imefikisha pointi 49 na kubaki katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa imecheza michezo 22.

Timu hiyo inazidiwa pointi tisa na vinara wa ligi hiyo Yanga yenye pointi 58.

Mchezo wa jana ulikuwa na kasi kwa timu zote mbili baada ya kushambuliana kwa zamu, lakini washambuliaji wao walikosa maarifa ya kufunga mabao.

Washambuliaji wa Azam wakiongozwa na Donald Ngoma, waliendeleza ubutu katika safu yao licha ya kuwepo nyota wengine wa kigeni Obrey Chirwa na Tafadzwa Kutinyu.

Matokeo ya michezo mingine iliyochezwa jana Tanzania Prisons iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Stand United, Ndanda ilishinda mabao 2-0 ilipovaana na Kagera Sugar.

Katika mchezo mwingine wa mashindano hayo Ruvu Shooting ilitoka suluhu na African Lyon.