Azam v Singida United yaipisha Simba, AS Vita Jumamosi

Wednesday March 13 2019

 

By CHARITY JAMES

Dar es Salaam. Mechi ya Ligi ya Mabingwa kati ya Simba dhidi AS Vita umesababisha kurudishwa nyuma kwa siku moja mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) kati ya Azam FC na Singida United, uliokuwa ufanyike Jumamosi sasa utachezwa Ijumaa.

Mchezo huo wa ligi ulipangwa kucheza Jumamosi sasa utapigwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku lengo ni kuwapa nafasi mashabiki wa soka kwenda kuipa sapoti Simba Jumamosi Taifa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), imefanya mabadiliko hayo kutokana na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, kati ya Simba na AS Vita ya Congo kufanyika Jumamosi hii kwenye muda sawa na ule ambao mechi ya Azam FC dhidi ya Singida ingefanyika.

Meneja wa Azam FC, Phillip Alando alisema wamepata barua ya mabadiliko hayo na wanaendelea na maandalizi kuelekea mchezo huo.

Alisema maandalizi yao yanakwenda vizuri na nyota wao wote wapo katika ari nzuri ya mchezo na kuweka wazi kuwa hawana majeruhi yeyote ambaye amecheza michezo ya hivi karibuni hivyo wanaamini wataendelea na ushindi katika mchezo huo.

Kikosi cha Azam FC kipo kwenye mwenendo mzuri hivi sasa baada ya timu hiyo kushikwa na makocha wazawa, Idd Nassor Cheche na Meja Mstaafu, Abdul Mingange wanafundisha kwa muda wakitoka katika timu za vijana za matajiri hao.

Advertisement