Azam yamiliki mpira asilimia 70, shuti goli 0, yachapwa bao 1-0

Muktasari:

Azam iliingia na mbinu ya kushambulia, lakini baadaye walianza kupunguza mashambulizi hali iliyowaruhusu wapinzani wao kufunguka na kuanza kushambulia.

Dar es Salaam. Azam imeweka rekodi pamoja na kumiliki mpira kwa asilimia 70, imeshindwa kupiga shuti hata moja lililolenga goli ikichapwa bao 1-0 na Triangle United ya Zimbabwe katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Kocha Ettiene Ndayiragije alishindwa na mbinu za mchezo huo kutokana na wapinzani wake Triangle kucheza mpira wa kujilinda muda wote huku wakishambulia kwa kushtukiza.

Ndayiragije alionja joto la mashabiki wa Azam wakati alipojaribu kumtoa Idd Seleman ‘Nado’ jambo lililofanya mashabiki hao kuzomea na kupinga hivyo kumfanya Mrundi huyo kubasilisha uamuzi kwa kumtoa Chilunda ambaye ndiyo kwanza alikuwa ameingia na Nado kuendelea na mchezo.

Katika mchezo huo Azam ilianza kwa kasi tangu dakika ya kwanza kwa kulishambulia lango la Wazimbabwe hao, lakini washambuliaji Richard Djodi na Chirwa walikosa umakini.

Dakika ya 18 Obrey Chirwa alikosa goli baada ya kupigiwa pasi na Idd Nado na kuingia na mpira ndani ya boksi, lakini umaliziaji ulikuwa tatizo kwake.

Dakika 28 Azam ilipata faulo kupitia kwa Frank Domayo ambapo wachezaji wa Azam walipigiana pasi za haraka haraka na kiungo huyo kupenya kuingia ndani ya boksi na kufanyiwa madhambi lakini faulo hiyo iliyopigwa na Richard Djodi haikuwa na madhara.

Azam walionekana kuingia na mbinu ya kushambulia, lakini baadaye walianza kupunguza mashambulizi hali iliyowaruhusu wapinzani wao kufunguka na kuanza kushambulia.

Dakika 33 Triangle nusura wapate goli la kuongoza kupitia faulo iliyotokana na mshambuliaji wa Azam, Richard Djodi kufanya madhambi nje kidogo ya boksi lao.

Faulo hiyo iliyopigwa na Praise Tonha ilipanguliwa vizuri na kipa wa Azam, Razack Abarola hata wachezaji wa Triangle walipowahi mpira huo walishindwa kufanya kitu.

Dakika 34, Triangle ilipata bao la kwanza kupitia kwa Ralph Kawondera ambaye alitumia vizuri makosa ya kipa wa Azam, Razack Abarola ambaye alitaka kuudaka mpira na kupishana nao baada ya kuchanganyana na mabeki wake huku mshambuliaji Kawondera akikutana na mpira na kuuweka moja kwa moja wavuni.

Katika kipindi cha pili Azam ilifanya mabadiliko dakika 59 kwa kumtoa Richard Djodi na kuingia Shaban Chilunda.

Dakika 63 Praise Tonha wa Triangle alipewa kadi ya njano baada ya kumfanyia madhambi Obrey Chirwa.

Azam ilionekana kuhitaji goli la kusawazisha, lakini mipango yao ilionekana kukwama kila wanapofika langoni kwa Triangle.

Dakika 68 winga Idd Nado aliwatoka mabeki wa Triangle na kuachia shuti kali lakini liltoka pembezoni kidogo na goli.

Nado alionekana kufahamu njia mbadala ya kupita mabeki wa Triangle baada ya kufanya shambulizi lingine kwa kupiga shuti akiwa nje ya 18, lakini bado mpira ulikuwa unapita pembezoni mwa goli.

Dakika 73 Azam ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Shaban Chilunda ambaye alicheza dakika 13 tu katika mchezo huo na nafasi yake kuchukuliwa na Idd Kipagwile.

Triangle nao walifanya mabadilko kwa kumtoa na kuingia Tinashe Chivandire wakati huohuo Azam walimtoa Emmanuel Mvuyekure na kuingia Mudathir Yahya.

Triangle ilifanya mabadiliko mengine dakika 83 walifanya mabadiliko ya kumtoa Allan Tavarisa na kuingia Simba Makoni.

Mabadiliko ya Azam hayakuonyesha kuwa na tija katika kikosi chao kwani bado walishindwa kabisa kuingia na kupata bao la kusawazisha.