Banda awapa mzuka Taifa Stars

Muktasari:

  • Kikosi cha Taifa Stars kina wachezaji 10 wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi ambao ni nahodha wake Mbwana Samatta anayekipiga KRC Genk ya Ubelgiji, Saimon Msuva (Difaa El Jadida/ Morocco na Rashid Mandawa wa BDF ya Botswana.

Dar es Salaam. Beki wa Baroka FC ya Afrika Kusini, Abdi Banda amekitakia kila la kheri kikosi cha Taifa Stars kwenye mchezo wake wa leo wa kuwania kufuzu Fainali za Afrika (Afcon) mbele ya Uganda.

Banda, 23, ni miongoni mwa wachezaji wa Kitanzania wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi ambao hawakupata nafasi ya kuitwa kwenye kikosi hicho kinachonolewa na Mnigeria Emmanuel Amunike.

Beki huyo wa kati alisema amekuwa akiwasiliana na wachezaji wenzake ambao wameitwa kwenye kikosi hicho kama sehemu ya kuwahamasisha ili waweke rekodi kwa taifa. “Tumekuwa wasindikizaji wa wenzetu kwa miaka mingi, dua zetu zipo kwao, kila Mtanzania kwa sasa anaitakia mema Taifa Stars, ushindi wao utatufanya tutembee vifua mbele.

“Kila mmoja wetu atajivua taifa lake. Niwaombe Watanzania wajitokeze kwa wingi Uwanja wa Taifa kwa ajili ya kuwapa nguvu wachezaji ili wafanye kile ambacho tunakitarajia, shabiki ni mchezaji wa 12 na ana nafasi kubwa kwenye soka,” alisema.

Kikosi cha Taifa Stars kina wachezaji 10 wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi ambao ni nahodha wake Mbwana Samatta anayekipiga KRC Genk ya Ubelgiji, Saimon Msuva (Difaa El Jadida/ Morocco na Rashid Mandawa wa BDF ya Botswana.