Bao la Nchimbi laiua Zanzibar, Kilimanjaro Stars yafufuka Chalenji

Tuesday December 10 2019

 

By Charles Abel

Kampala, Uganda. Bao pekee la mshambuliaji Ditram Nchimbi limetosha kuipa timu ya taifa ya Tanzania Bara 'Kilimanjaro Stars' ushindi 1-0 dhidi ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes' katika mashindano ya Chalenji inayoendelea kwenye Uwanja wa KCCA, Uganda.

Nchimbi alifunga bao hilo katika dakika ya 38 akimalizia mpira uliotemwa na kipa Suleiman Ali baada ya shuti la Eliuter Mpepo.

Matokeo hayo yanafufua matumaini Kilimanjaro Stars kufuzu kwa nusu fainali baada ya kufikisha pointi 3, wakati Zanzibar ikiwa na pointi moja hivyo timu zote mbili zitalazimika kushinda katika mechi zao za mwisho dhidi ya Sudan na Kenya.

Katika mchezo huo, timu hizo zilicheza kwa kushambuliana ambapo Zanzibar ilikuwa ya kwanza kufanya shambulizi la mapema dakika ya pili kupitia kwa Kassim Khamis ambaye alipokea pasi ya Mudathir Yahya ndani ya eneo la hatari, lakini akiwa anamtazama Aishi Manula alipiga shuti lililopanguliwa na kipa huyo na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Zanzibar waliendelea kutawala mchezo katika dakika 20 za mwanzo lakini kutolewa kwa Mudathir Yahya aliyeumia dakika ya 30 kuliwagharimu kwani walijikuta wakiwa dhaifu katikati mwa uwanja, jambo lililowapa mwanya Kilimanjaro Stars kurudi mchezoni na kuanza kutawala mchezo.

Makosa ya kipa Suleiman Ali wa Zanzibar kupangua vibaya shuti la Mpepo, yaliizawadia bao Stars kupitia kwa Nchimbi ambaye aliunganisha mpira huo kwa shuti la mguu wa kulia lililojaa wavuni.

Advertisement

Mara baada ya kuingia kwa bao hilo wachezaji wa Zanzibar Heroes walimzonga mwamuzi Therry Nkuruzinza wa Burundi wakidai mchezaji Haruna Abdallah alifanyiwa madhambi na Mzamiru Yassin.

Advertisement