Kocha Biashara United afichua mkataba wake Yanga ulivyofutwa

Mwanza. Biashara United ni moja ya timu inayofanya vizuri katika Ligi Kuu Bara, huku wadau na mashabiki wakijiuliza sababu ya mafanikio hayo kulinganisha na msimu uliopita.

Timu hiyo ambayo awali ilijulikana kama Polisi Mara kabla ya kubadilishwa na kuitwa Biashara United, ilianza msimu huu ikiwa chini ya kocha Amri Said ‘Stam’.

Msimu uliopita timu hiyo ilinusurika kushuka daraja kwa madai ya maisha magumu na kusababisha aliyekuwa kocha wake, Hitimana Thiery kuondoka na mikoba yake kuchukuliwa na Stam.

Msimu huu Biashara imeonekana kuwa tishio tangu alipopewa majukumu kocha Francis Baraza ambaye katika michezo 17 amepoteza mitatu tu.

Alikotoka

Akizungumza na Spoti Mikiki, Baraza anasema maisha yake yote amekuwa ni mtu wa mpira kwani hata familia anayotoka ilikuwa ni watu wa mpira kuanzia baba yake hadi ndugu zake.

Anasema wamekuwa watu maarufu Kenya kutokana na kazi ya mpira, lakini hata huko alikosoma shule za msingi na sekondari alilelewa na watu wa soka.

Ushindani

Kocha huyo anasema licha ya kupitia timu nyingi, lakini rasmi aliingia kwenye soka la ushindani mwaka 1989, alipoanza kuichezea timu ya Nyota FC kwa miaka minne ikiwa Ligi Daraja la Pili.

Anasema kiwango chake kilikuwa bora na kumvutia kila kocha aliyekuwa akikutana naye kwani aliweza kuisaidia kupanda Ligi Kuu

Anasema baada ya kudumu miaka minne katika kikosi cha Nyota alihamia Transcom aliyokaa kwa msimu mmoja kabla ya kujiunga na Rivertex kwa miaka mitatu mwaka 1993-1996.

Anasema licha ya kucheza nafasi ya beki pia alikuwa mfungaji hodari wa mabao. Mwaka 1996 alijiunga na AFC Leopards ambayo aliitumikia misimu miwili kabla ya kujiunga na Shabana na mwaka 1999 Yanga ilimtupia ndoano.

Yanga

Kocha huyo anasema mwaka 2000 wakati Kenya ikicheza na Tanzania michuano ya Cecafa, mmoja wa vigogo wa Yanga alikuwa akifuatilia mchezo kwa umakini ili kuondoka na wachezaji watakaoungana na timu hiyo.

Anasema katika mchezo huo kigogo huyo alivutiwa na yeye na mshambuliaji Vincent Tendwa.

Baraza anasema moja ya tukio ambalo hadi leo hatasahau katika maisha yake ni kutibuliwa dili lake la kucheza Yanga kwani alikuwa tayari ameshatia saini mkataba.

Anasema ndoto yake ilikuwa ni kucheza Yanga na ikiwa tayari ameshamwaga wino wa miaka miwili kuitumikia, lakini mabosi wa Shabana walitibua mipango yake.

Anasema alikuwa ameshamaliza mkataba na Shaban, lakini uongozi ulikuwa unahitaji kuendelea naye ingawa akili yake ilikuwa ni kucheza Yanga.

“Haiwezi kusahaulika kirahisi ilikuwa mwaka 2000 niliposajiliwa Yanga kwa mkataba wa miaka miwili, lakini Shabana ikanifanyia hujuma hadi nikakosa nafasi hiyo” anasema kocha huyo.

Anasema kwa kipindi alichokuwa amejiunga na Yanga alicheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya Bandari ya Mtwara na kufunga mabao mawili kwa kichwa.

“Aliyekuwa mmoja wa wakurugenzi wa Shabana (jina tunalihifadhu) alinishawishi ataninunulia shamba niachane na Yanga nilipokataa ndio akashirikiana na baadhi ya viongozi wa Shirikisho la Soka Kenya wakagushi nyaraka kwamba bado nina mkataba,” anasema.

Rekodi

Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Kenya, anasema anachofanya Biashara ni mwendelezo wa mafanikio yake katika soka tangu akiwa mchezaji.

Akiwa mchezaji aliipandisha Nyota kutoka Daraja la Pili hadi Ligi Kuu, akaiwezesha timu ya taifa ya vijana katika Kombe la Chalenji kushika nafasi ya tatu mwaka 1994.

Anasema mwaka 1994 aliiwezesha Rivertex kubeba ubingwa wa Moi Golden na mwaka 1996, akiwa AFC Leopards wakati ule wa Ligi Kuu Kenya na Kombe la Cecafa.

“Baada ya kuhamia Oserian Fastac FC nilichangia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Kenya misimu mitatu mfululizo 2001-2003 na kumaliza michuano ya Cecafa nafasi ya pili mwaka 2002,” anasema Baraza.

Baraza anaeleza kuwa mwaka 2005 baada ya kustaafu soka akapewa jukumu kuinoa Sony Sugar na kuweka historia ya kutofungwa nyumbani. Akiwa kocha huko Kenya aliipa ubingwa Sony Sugar mwaka 2006.

Malengo

Baada ya kupewa mchongo wa kazi Tanzania na mmoja wa waliokuwa wachezaji wake alikuja kuonyesha uwezo wake. Baraza anajivunia mafanikio Biashara, aliikuta ikiwa nafasi ya 19 na sasa ipo nafasi ya 10 kwa pointi 40 na malengo yake ni kumaliza ligi katika nafasi sita za juu.

Anasema kwa uwezo na uzoefu alionao anaamini ataisaidia timu hiyo na kwamba kazi yake ni kufundisha soka na amekuja kufanya kazi Tanzania.