Barua nzito ya GSM kwa Yanga yaleta utata

Dar es Salaam.NYOTA wa Yanga wamevurugwa baada ya kusikia bilionea wa klabu hiyo Kampuni ya GSM kutishia kujiondoa kwenye baadhi ya huduma walizokuwa wakijitolea nje ya mkataba ikiwamo kambi na posho za wachezaji.

GSM kupitia Mkurugenzi wa Miradi, Feisal Mohamed waliuandikia barua uongozi wa Yanga jana Jumanne kueleza kujiweka pembeni kwenye ishu walizokuwa wakijitolea kwa hiari yao kama kusajili na kugharamia kambi kutokana na mzozo ulioanza kuibuka chini kwa chini.

Jambo hilo limewafanya wachezaji kuhamaki na kutaka viongozi wa klabu hiyo kukaa chini na kulimaliza kwa hofu wasirejeshwe kule kwenye maisha waliyoishi siku  nyuma ya kutegemea bakuli la kuombea michango kutoka kwa wanachana na wadau wa klabu.

Baadhi ya wachezaji wa Yanga walioomba kuhifadhiwa majina waliliambia Mwanaspoti kuwa, taarifa waliyoiona ya GSM kutaka kujiengua imewachanganya kwa vile ujio wa kampuni kama mmoja wa wadhamini wa klabu hiyo imewafanya waishi kwa amani na kucheza bila presha.

“Hapo nyuma kusema kweli hali ilikuwa mbaya sana, alipokuja huyu jamaa hata malazi hotelini tukabadilisha awali tulikuwa tunakaa Manzese baada ya kuja hao tumepelekwa Mikocheni, pia mishahara na posho tulikuwa tunapata kwa wakati japokuwa mambo ya kibinadamu utokea,” alisema mmoja ya nyota wa timu hiyo anayecheza eneo la kiungo.

Naye mmoja wa mabeki wa klabu hiyo alisema wamesikitishwa na taarifa hiyo na kwenda mbali zaidi kwa kusema, hata michezo ya Ligi ilichagizwa na ile ahadi ya Sh 200 milioni ambapo kila mchezaji alikuwa na uhakika wa kubeba Sh 10 milioni, mbali na ahadi ya Sh 10 milioni ya kila mechi ambapo wachezaji walipambana kuhakikisha wanaipata.

“Viongozi wetu kuna mahali huenda wameteleza, sisi tunachoomba kama wachezaji ni kutaka wayajenge na wenzao maisha yaendelee, ila sikufichi akitoka huyu jamaa Yanga patakuwa pazito kwa sababu wachezaji kwa sasa hatuna presha na stresi kama zamani." alisema nyota mwingine.

VIONGOZI WAUCHUNA

Hakuna kiongozi wa Yanga alikuwa tayari kuzungumzia sakata hilo, ambalo hata hivyo jioni hii zimeenea taarifa mmoja wa vigogo wa serikalini ameamua kuingilia kati na kutuliza mdudu mbaya aliyekuwa akitaka kuvuruga mambo wakati Ligi Kuu Bara ikielekea ukingoni.

MAJUKUMU YAKE GSM

Katika mkataba na Yanga GSM jukumu lake kubwa ilikua jezi pamoja na ukarabati wa jengo la klabu hiyo, ukarabati wa ofisi, Swimming sabamba na ujenzi wa uwaja wa mazoezi na duka la kisasa la kuuza vifaa vya michezo klabuni hapo.

Lakini kutokana na mapenzi ambayo GSM alikuwa nayo kwa Yanga alifanya mambo mbalimbali ambayo ni kinyume na mkataba wake na sasa yanamtokea puani.

YALIYOKUWA HAYAMUHUSU

Miungoni mwa mambo ambayo aliyafanya kinyume na mkataba niKumrejesha kundini Lamine Moro aliyekuwa akitaka kutimka kunako klabu hiyo, kufanya usajili wenye tija kwa wachezaji Bernard Morrison, Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima pamoja na Adeyun Salehe ambao ni tegemeo kwa sasa ndani ya timu hiyo.

Kuwaleta na kuwalipa gharama zote kocha mkuu, wa mazoezi na wa viungo ambapo ni pamoja na mishahara, usafiri wa ndani nyumba, tiketi za kwenda na kurudi makwao.

Kulipa mishahara, malipo ya bonasi kutokana na ushindi, gharama za kambi, hotel kuanzia Desemba, tiketi za ndege kwa wachezaji na viongozi.

Gharama za uwanja wa mazoezi, pamoja na ununuzi wa vifaa vya mazoezi, kulipa madeni ya nyuma ya usajili wa wachezaji, gharama za kuwaleta watu kwa ajili ya kuanza mchakato wa mfumo mpya.

NUGAZ APOTEZEA

Alipotafutwa Antonio Nugaz ambaye ndiye aliyekuwa akizungumzia mara kwa mara mambo yahusuyo mdhamini huyo na hata walipokuwa wakitafutwa watu wa GSM walielekeza atafutwe Nugaz.

Kwa leo mambo yalikuwa si mambo, kwani  alipopigiwa aligoma kamwe kuzungumza lolote juu ya hilo na kuelekeza kijiti kwa Mkuu wa Idara ya Habari ya klabu hiyo Hassan Bumbuli ambaye naye alirusha mpira kwa Mwenyekiti wake, Dk Mshindo Msolla na Katibu Mkuu, Dk Davi Ruhago ambao hata hivyo hawakupatikana hewani.