Beki Morris arudi kikosini Azam

Wednesday October 9 2019

 

By DORIS MALIYAGA

Dar es Salaam. Beki wa Azam FC, Aggrey Morris ameanza mazoezi na wenzake huku akisisitiza hamu yake ni kuona wanatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Aggrey aliumia wakati wa mechi za maandalizi ya Fainali za Afcon Misri na kufanyiwa upasuaji wa goti na kumlazimisha kukaa nje ya uwanja kwa takribani miezi minne.

"Namshukuru Mungu naendelea vizuri kabisa na tayari nimeanza mazoezi, kidogo kidogo nitakuwa vizuri," alisema Aggrey.

Daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa alisema: "Aggrey ameshaanza mazoezi mepesi anaendelea vizuri."

Akizungumzia kikosi chake kuchukua ubingwa, Aggrey alisema: "Ligi kwa sasa imekuwa ngumu kama unavyoona kila timu tunayocheza nayo imekuwa ikitupa changamoto. Tumekuwa tunapata ushindi kwa nguvu sana sasa sijui ni sisi tu wanatupannia, lakini hamu yetu na yangu ni kuona msimu huu unakuwa wetu, tunachukua ubingwa."

Azam tangu ilipotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania msimu wa 2013-2014 chini ya Kocha Joseph Omog imeshindwa kurudia mafanikio hayo.

Advertisement

 

Advertisement