Beki wa Singida United atua Simba kumrithi Juuko

Muktasari:

Simba msimu ujao itakuwa na kazi ya kutetea ubingwa wake wa Ligi pamoja na kuhakikisha inafikia mafanikio ya msimu uliopita katika Ligi ya Mabingwa

Dar es Salaam. Mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba wameimalisha safu yao ya ulinzi kwa kumsajili beki wa kati wa Singida United, Kennedy Wilson Juma kwa mkataba wa miaka miwili.

Juma alisaini mkataba kabla ya kwenda kujiunga na kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars kwenye orodha ya wachezaji wa kwanza walioitwa kabla ya kwenda Misri.

Uongozi wa Simba umemsajili Juma ili kuongesa nguvu katika safu ya ulinzi lakini baada ya beki Mganda Juuko Murshid kutangaza kuachana na mabingwa hao.

Nahodha huyo wa Singida United alikuwa katika kikosi cha kwanza Taifa Stars kabla ya kuenguliwa katika orodha ya wachezaji 23 waliokwenda Misri Afcon.

Mwanaspoti wiki iliyopita lilikufichulia usajili wa Juma lilimtafuta na kueleza kwa ufupi kuwa amekuja Simba kushindana ili kuisaidia timu kufikia malengo yake.

"Simba ni timu kubwa nipo tayari kupambana na ushindani ambao nitakutana nao ili kupata nafasi ya kucheza na kuisaidia timu kufikia malengo yake," alisema Juma.