Benzema amfananisha Giroud na 'kigari kidogo'

Muktasari:

Olivier Giroud aliiongoza Ufaransa kutwaa Kombe la Dunia nchini Russia miaka miwili iliyopita, wakati Benzema hajaitwa kikosini tangu mwaka 2015 kutokana na kuhusishwa na njama za uhalifu.

Mchezaji wa Real Madrid, Karim Benzema amemkejeli mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa, Olivier Giroud kwa kujifananisha na dereva wa magari ya mwendokasi ya langalanga (Formula One), huku akimfananisha mshambuliaji huyo wa Chelsea na go-kart, magari madogo zaidi ya mashindano.
Benzema hajaichezea Ufaransa tangu mwaka 2015 na alikuwa mbali wakati Giroud akiiongoza nchi hiyo kutwaa Kombe la Dunia nchini Russia miaka miwili iliyopita.
Akiwa ameshaichezea Real Madrid zaidi ya mechi 500 katika msimu wake wa 11 na vigogo hao wa Hispania, hakuna maswali kuhusu uwezo wake.
Alipoulizwa kuhusu mshambuliaji huyo wa Chelsea katika kipindi cha maswali na majibu Jumapili usiku, Benzema alisema: "Huwezi kuchanganya gari la Formula One na la go-kart, na nakuwa mstaarabu. Najua mimi ni dereva wa gari la Formula One car...
"(Mambo) Yanakwenda kwa sababu yuko pale, hilo tu. Haitakuwa ya kuvutia. (Antoine) Griezmann na (Kylian) Mbappe wanaonekana zaidi wakati yeye akikunja mikono ya jezi na kufanya kazi chafu.
"Lakini kuna yeyote anayependa mchezo wake? Sijui."
Katika misimu ya 2016 na 2017 kabla ya fainali za Russia 2018, Giroud alifunga mabao 16 katika mechi 24 alizochezea Ufaransa.
Na pia alicheza kila mechi ya fainali za Kombe la Dunia ingawa alishindwa kuziona nyavu nchini Russia, timu yake ilirudi nyumbani na kombe.
Kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps amekuwa akimuacha Benzema tangu kesi yake ya kisheria ya mwaka 2015.
Kesi ilimuhusisha Benzema akituhumiwa kujaribu kufanikisha mpango wa kutaka kutumia kwa maslahi binafsi siri za mchezaji wa kimataifa wa Ufaransa, Mathieu Valbuena kuhusiana na filamu binafsi kwa kutumia simu iliyoibiwa.
Uchunguzi unaendelea na Benzema sasa anasubiri kama atatakiwa kujibu mashtaka ya uhalifu.
Benzema amefunga mabao 19 katika mechi 32 alizoichezea Real Madrid msimu huu wakati Giroud amekuwa akitumika zaidi kama mchezaji wa akiba.