Bifu la Mane na MO Salah limeanzia hapa...

LIVERPOOL ENGLAND. SUPASTAA Sadio Mane alionekana kuwa mwenye hasira baada ya mshambuliaji mwenzake Mohamed Salah kushindwa kumpa pasi wakati yeye akiwa kwenye nafasi nzuri ya kufunga kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu England ambapo Liverpool iliichapa Burnley 3-0 wikiendi iliyopita.

Staa huyo wa Senegal alitolewa muda mfupi tu baada ya tukio hilo, lakini hakuweza kuficha hasira zake, alionekana akibwatuka mbele ya benchi la ufundi na wachezaji wenzake kadhaa walimtuliza, akiwamo Roberto Firmino, Joe Gomez na James Milner.

Kocha Jurgen Klopp aliamua kulipuuzia jambo hilo, lakini video ya Roberto Firmino ikimwonyesha akicheka kutokana na jambo hilo ghafla ilipata umaarufu sana kwenye mitandao ya kijamii. Mashabiki nao wakavamia na kukuza mambo, wakidai kutakuwa hakuna uhusiano mzuri baina ya wawili hao, huku baadhi wakimshutumu Mo Salah kuwa ni mbinafsi.

Lakini huko nyuma mwezi Mei, muda mfupi kabla ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Mane alisema kitu kuhusu uhusiano wake na Mo Salah, katika mahojiano maalumu yaliyofanywa na gwiji wa Liverpool, Robbie Fowler. Haya ndiyo majibizano yao yalivyokuwa.

Fowler: Ok, swali hili nikiwa mshambuliaji mwenzako. Matokeo ni 0-0 hadi dakika ya mwisho ya mechi ya fainali, imepatikana nafasi. Nani ungetaka awe kwenye nafasi hiyo ya kufunga, wewe au Mo Salah?

Mane: Hahahaha! Mimi nataka ushindi tu! Mo anafunga, mimi nafunga, nahitaji kombe. Nadhani, ninachohitaji ni taji tu, wakati mwingine mambo mengi yamekuwa yakinikwaza. Anaweza kufunga, Mo wewe funga tu. Hadi tutakapopata taji, Mo afunge tu!

Fowler: Nadhani hili linafanya ufahamike zaidi jinsi ulivyo. Mimi sidanganyi, ningetaka niwe mimi!

Mane: Nataka kusema ukweli. Nataka taji, kama Mo yupo kwenye nafasi ya kumpunga nampa mpira, tunataka taji, hivyo afunge tu!

Fowler: Unaonekana kama ni mchezaji unayetaka kujitolea kwa ajili ya timu. Hivi unafurahia kwamba umekuwa huzungumziwi sana, wakati Mo anapata sifa tu kila siku, wewe unaichukuliaje hiyo?

Mane: Nadhani tangu msimu uliopita, hadi wakati huu, Mo amekuwa kwenye kiwango bora sana. Kama unataka kushinda kitu kwenye timu, bila ya shaka unahitaji wachezaji wa aina hii. Hiyo unatumia nguvu iliyopo kwenye timu. Mo alikuwa mfungaji bora, alikuwa akifunga na kutusaidia. Kama asingekuwapo, pengine tusingefika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, kwa sasa amekuwa akifunga mabao mengi muhimu.

Kwangu mimi muhimu ni kushinda kitu. Mo anaweza kufunga, au Bobby Firminho au mimi, haijalishi. Nadhani kama timu tumekuwa tukifanya kila kitu kitimu, tunasaidiana. Kipa, mabeki, viungo, kila mmoja.

Fowler: Watu wanasema huko kuna ushindani mkubwa baina yetu na hamna urafiki kabisa, kweli hakuna tatizo hapo?

Mane: Hakuna. Maneno kama hayo au vitu vingine vyovyote vimekuwa vikitokea sana kwenye soka. Mimi sijali, kama nimefunga au sijafunga ilimradi timu imeshinda. Baadhi ya watu wanataka kusema tuna upinzani, lakini nadhani hilo ndilo linalofanya mchezo wa soka uwepo, upinzani.

Lakini, hilo halina maana kwangu. Kwa kusema ukweli!