Bigirimana kikaangoni Yanga

Muktasari:

Kwa upande wake, Mkwasa alisema msafara wa wachezaji 20 wa Yanga, utaondoka leo alfajiri kwenda Mwanza kwa ajili ya mchezo wao na Alliance utakaofanyika Ijumaa.

Dar es Salaam. Kaimu kocha mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa, amemzuia kiungo mshambuliaji, Issa Bigirimana kutofanya mazoezi hadi atakapotoa sababu za kuchelewa kujiunga na timu.

Bigirimana aliondoka nchini mara baada ya mchezo wao dhidi ya Ndanda ambao, aliingia kipindi cha pili na kucheza kwa dakika tano kisha kuomba ruhusa ya siku tatu kurudi nchini kwao.

Afisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema Bigirimana alirejea nchini jana na alishindwa kufanya mazoezi na wenzake kutokana na Mkwasa kuhitaji kwanza maelezo ya sababu za kuchelewa kujiunga na timu.

“Bigirimana karudi (juzi) na jana hakufanya mazoezi, lakini uongozi umempa onyo na kumtaka ajieleze sababu za kuchelewa,” alisema.

Kwa upande wake, Mkwasa alisema msafara wa wachezaji 20 wa Yanga, utaondoka leo alfajiri kwenda Mwanza kwa ajili ya mchezo wao na Alliance utakaofanyika Ijumaa.

Alisema kwenye msafara huo hatakuwa na wachezaji wake wanne viungo: Feisal Salum, Abdulaziz Makame, Mapinduzi Balama na Mohamed Issa Banka.

Feisal, Banka na Makame wamejiunga na kambi ya timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) inayojiandaa na michuano ya Chalenji inayotarajiwa kufanyika nchini Uganda huku Mapinduzi akiwa majeruhi.

“Wachezaji wako vizuri na wana ari ya ushindani, tutasafiri na wachezaji 20 na wale ambao hawatakuwepo ni kwa ruhusa maalumu.

“Tumeshindwa kuwarudisha wachezaji hawa kwa sababu wameingia kambini moja kwa moja. Awali, ratiba haikuwa ikituonyesha kuwa na mechi hadi Januari 4 dhidi ya Simba, lakini sasa tunamichezo miwili Mwanza na Dar es Salaam dhidi ya KMC,” alisema Mkwasa.