Billioni 20 za Mo Dewji hazijaguswa

KAIMU Mwenyekiti wa Simba, Mwina Kaduguda amewatoa hofu wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kuwa zile fedha za uwezekzaji za Mohammed ‘Mo’ Dewji, Sh 20 Bilioni hazijaguswa.

Kadugunda amesema Mo Dewji ameshawekeza mabilioni kwenye klabu hiyo, lakini hazijaanza kutumika kwa vile wamejitengenezea mfumo unaowaingizia fedha za kujiendesha bila kuzigusa wakisubiri mchakato wa klabu yao kuwa kampuni ukamilike.

Kaduguda amelazimika kutoa ufafanuzi huo kutokana na minong’ong’ono kuhusiana na uwekezaji wa klabu hiyo ambao umeonekana kama zoezi hilo limekuwa kimya na kuchukua muda mrefu.

Alisema kuwa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba kwa sasa inafanya mchakato huo na serikali baada ya kukamilika kutoka kwa wanachama waliopitisha mchakato huo.

“Sisi tunafanya kazi na serikali na kuna masuala ambayo yanatakiwa kufanyika ili kufikia hatua ya kutangaza mchakato uliokamilika. Unahitaji kuwa na subira,” alisema Kaduguda.

Alisema pamoja na MO kuweka fedha hizo, bado hazijaanza kutumika na kilichofanyika ni kuwekeza fedha hizo katika mfumo maalum na kuingizia klabu hiyo kati ya Sh 1.5-2 Bilioni kwa mwezi na kutumika katika uendeshaji wa klabu.

Aliongeza Sh 20 Bilioni zitaanza kutumika mara klabu hiyo itakapo kamilisha mfumo wa kutoka kwenye uongozi wa Kamati ya Utendaji na mfumo wa uongozi wa bodi.

“Huwezi kuanza kutumia Sh 20 Bilioni za uwekezaji wakati bado kuna michakato mbalimbali haijakamilika, haitakuwa sawa kabisa,” alisema.

Alifafanua, mchakato kukamilisha mfumo huo unaendelea kwa umakini zaidi na lengo lao ni mfumo mzuri wa uongozi na hata akija kiongozi mwingine atafuata mfumo huo.

Kwa mujibu wa Kaduguda, mchakato wa kukamilisha mfumo wa uendeshaji unatakiwa kuwa na umakini zaidi na zoezi ambalo linahusisha vyombo vya serikali kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Tume ya Taifa ya ushindani (FCC).

“Kuna mambo mengi kwa sasa uongozi wa Simba unayafanya sambamba na mfumo wa uwekezaji. Tunataka mtu akija kuongoza klabu anakuta kila kitu kipo sawa. Ukihitaji mahesabu na mambo mengine, utayapata na siyo vinginevyo,” alisema katibu huyo wa zamani wa TFF.

“Lazima tuondoke kwenye mfumo wa uongozi wa mazoea, tunataka mfumo wa kisasa ambao kiongozi mwingine akichaguliwa kwa mujibu wa katiba na kutaka kuingiza mambo tofauti, ataulizwa ameyatoa wapi hayo,” alisema Kaduguda.

Alisema mchakato huo ukikamilika, Simba itakuwa miongoni kwa timu zilizopiga hatua kubwa sana barani Afrika kama vile TP Mazembe, Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na klabu nyingine kubwa katika bara la Afrika.

NAFASI YA KAIMU MWENYEKITI

Kaduguda alisema amekaimishwa kushika nafasi ya hiyo hadi hapo Simba itakapofanya Uchaguzi Mkuu mwaka 2022.

Alisema alikaimishwa katika nafasi hiyo katika mkutano wa wanachama uliofanyika Desemba 8 mwaka jana na kuongeza kwa mujibu wa Katiba ya Simba hairuhusu zoezi la kufanya uchaguzi wa kuziba nafasi hiyo ambayo iliachwa baada ya aliyekuwa Mwenyekiti, Swedi Mkwabi kujiuzulu.