Boca Juniors yaagwa Kifalme ikienda Hispania

Wednesday December 5 2018

 

Buenos Aires, Argentina. Watu wameacha kazi zao maduka kufungwa na shughuli katika jiji la Buenos Aires, zilisimama kwa muda baada ya mashabiki wa Boca Juniors, kufanya maandamano wakiiaga timu yao ilipoanza safari ya umbali wa maili 6000 kuelekea mjini Madrid, Hispania.

Timu hiyo kutoka Amerika ya Kusini, inaenda Hispania kwa ajili ya mechi ya pili ya Fainali ya Superclasico Copa Libertadores dhidi ya mahasimu wao wa jadi River Plate mchezo utakaochezwa Uwanja wa Santiago Bernabeu, Jumapili hii.

Mechi hiyo imelazimika kuhamishwa kutoka Amerika ya Kusini hadi Barani Ulaya kuepuka mauaji yanayoweza kutokea kutokana uhasama uliopo.

Mashabiki wa Boca Juniors waliapa kulipiza kisasi kwa kilichotokea Novemba 24 ambapo mechi ya marudiano ilifutwa baada ya mashabiki wa River Plate kulipopowa kwa mawe basi la Boca Juniors.

Tukio hilo la shambulizi la kushitukiza lilisababisha basi hilo  kuvunjwa vioo huku wachezaji wawili wakijeruhiwa usoni akiwemo mshambuliaji Carlos Tevez.

Katika mechi ya kwanza ya fainali timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2, Serikali imebariki uamuzi wa Chama cha Soka Argentina kuihamishia mechi hiyo barani Ulaya.

Katika mchezo wa kwanza wa Fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa La Bombonera, Boca Juniors ikiwa mwenyeji ililazimishwa sare ya mabao 2-2 na River Plate.

Wakilenga kuihujumu timu hasimu na kupata matokeo mashabiki wa River Plate wakaamua kuwasaidia wachezaji wao kwa kuwapopowa kwa mawe wapinzani wakilenga kuwaumiza ili wasiweze kufanya vema uwanjani.

Advertisement