Bocco: Tuna deni kubwa Simba

Nahodha wa Simba, John Bocco amesema imebaki upande wao kulipa deni kwa viongozi na wanachama wao ili kuweka heshima kwenye klabu yao.
Deni kubwa ambalo Bocco amelitamka kwamba ni kuhakikisha wanatetea ubingwa ili warejee kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo msimu huu walitolewa hatua ya awali.
Bocco alisema viongozi wao na mashabiki wamekuwa wakifanya kazi kubwa kwao kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa ikiwemo ujenzi wa uwanja wao wa Bunju.
Amesema kuwa watahakikisha wanafanya kila jitihada ili kutetea ubingwa wao na kuifunga Yanga kama mchezaji wa Simba wa zamani, Maloto Somo alivyotaka kuhakikisha wanawafunga watani wao.
"Hili ni deni kubwa sana kwetu, viongozi na wanachama wamefanyakazi kubwa sana juu yetu hivyo ni lazima tuhakikishe tunaafanya yote yaliyo mazuri kwao," amesema Bocco
Nahodha huyo amewaeleza Wanasimba kwamba wamesikia rekodi za wachezaji wao wa zamani kama Abdalah Kibadeni ambaye aliifunga Yanga hat-trick na ubora wa Malota kwamba kila mmoja ndani ya Simba anatakamani mafanikio hayo.
"Sitaki kujisemea mimi juu ya rekodi yangu kwani naamini ndani ya Simba kila mmoja ana uwezo mkubwa wa kucheza soka na kuweka rekodi. Tunaamini tutavunja rekodi zao.
"Hivyo bado tunaomba sapoti yenu na pia viongozi wa zamani kuendelea kutoa ushauri kwa viongozi wa sasa," alisema Bocco.