Bocco aifumua Simba SC mabosi wahaha, Mbrazili majanga

Muktasari:

  • Bocco hajaonekana uwanjani tangu alivyoumia katika mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam waliyoilaza mabao 4-2.

MABOSI ya Simba wamekiangalia kikosi chao kwa sasa na kubaini kama hawatajipanga mapema wanaweza kupata aibu Januari 4 watakapovaana na watani zao, Yanga katika mechi ya Ligi Kuu Bara.

Ishu nzima ni kuhusiana na nahodha wao John Bocco aliye majeruhi na kumuachia msala, Meddie Kagere ambaye kama akibanwa na mabeki, Simba hukosa maarifa mengine, kwani Mbrazili wao, Wilker Da Silva naye ana majanga yake.

Bocco hajaonekana uwanjani tangu alivyoumia katika mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Azam waliyoilaza mabao 4-2.

Tangu awe majeruhi amekuwa akipata matibabu katika hospitali kadhaa nchini pamoja na madaktari wa timu hiyo, Yassin Gembe na Paul Gomez, lakini kupona kwake kumekuwa ishu na sasa uongozi umeamua kumpeleka Afrika Kusini ili kupata tiba zaidi ili arejee mapema uwanjani.

Kukosekana kwa Bocco na Da Silva kumefanya Simba imtegemee Kagere kama straika pekee, jambo ambalo linamchanganya Kocha Patrick Aussems.

Kocha Aussems alisema anafahamu Bocco anaendelea na matibabu, ila hajua muda gani atakaokuwa nje kuuguza majeraha yake mpaka hapo atakapokuwa tayari kumtumia kwenye mechi.

Aussems alisema Da Silva hakumtumia katika mechi za nyuma kwani tangu apone hakuwa fiti kabla ya kutonesha tena walipokuwa wakijiandaa dhidi ya Prisons na atakuwa nje kwa muda.

“Kwa maana hiyo naendelea kubaki na mshambuliaji mmoja kwenye kikosi changu, Kagere, ambaye kama ikitokea amepata shida nakuwa sina mbadala wake, kwa maana hiyo nimewaomba viongozi kadri ambavyo wanaweza wakati wa dirisha dogo waongeze straika mwingine,” alisema Aussems.

Bocco aliyesajiliwa Simba misimu miwili iliyopita na kuifungua karibu mabao 30 katika Ligi Kuu, alikuwa akishirikiana na Kagere katika michuano mbalimbali, jambo linalomfanya Aussems kufikiria kupangua kikosi kwa sasa ili kuweka mambo sawa.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa alisema kutokana na vipimo alivyofanyiwa Bocco inaonyesha jeraha lake sio la muda mfupi, bali mrefu na wamepanga kumpeleka Afrika Kusini kwa matibabu zaidi ambayo baada ya muda mfupi wataeleza kinachoendelea.

“Tupo katika mpango huo wa kumpeleka nje ya nchi Bocco ili kupata matibabu ambayo nina imani yataeleza ambacho anatakiwa kufanyiwa na muda gani ambao atakuwa nje tofauti na vile vipimo ambavyo vilifanyika hapa nchini, na mpaka sasa hajaweza kurejea,” alisema.

“Kuhusu Wilker jeraha lake sio kubwa na wala hatakwenda Afrika Kusini kama ilivyo kwa Bocco, wala kufanyiwa upasuaji kwani matibabu ambayo atayapata hapa yatamtosha na atarejea uwanjani baada ya muda mfupi.”

WASIKIE HAWA

Kutokana na utata wa mastraika Simba, Mchambuzi wa soka nchini, Edo Kumwembe alisema kwa sasa Msimbazi wanahitaji straika mwenye uwezo wa kufunga tu na sio ‘kupaka rangi’ kwani wachezaji wa aina hiyo wanao wengi - tena wana uwezo wa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga.

“Mastraika kwa hapa ndani ambao Simba wanaweza kufiti kwenye timu yao ni yule wa Azam, Richard Djodi au Ditram Nchimbi, lakini kama wakitoka nje ya nchi kama Zimbabwe na nchi nyingine soko ni kubwa,” alisema Kumwembe.

Mchezaji wa zamani wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’ alisema kwa alivyokiangalia kikosi hicho kuna haja ya kuongeza straika ambaye ataingia kikosi cha kwanza moja kwa moja na sio kuanza kujaribiwa au kupewa muda.

“Nadhani kwa aina ya mshambuliaji ambaye wanamtaka Simba anatakiwa aliyekamilika katika uwezo wa kufunga zaidi ya waliokuwepo sasa, lakini wakileta aliye chini zaidi ya hapo tutaendelea kuwaona wakipata shida eneo hilo,” alisema.

“Kikosi chao kilivyo nadhani wachezaji kama Cletous Chama, Sharaf Eldin Shiboub, Miraji Athumani, Ibrahim Ajibu na Hassan Dilunga wanaweza kucheza nyuma ya mshambuliaji ingawa watakosa baadhi ya sifa za mshambuliaji asilia.”