Bocco aipania Yanga SC Kombe la Mapinduzi leo

Friday January 6 2017

 

By Oliver Albert, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Nahodha wa Azam FC, John Bococo amesema hawana budi kukomaa kuhakikisha wanaifunga Yanga leo ili waingie nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi.

Tayari, Yanga imefuzu hatua hiyo kutoka kundi hilo lenye timu za Azam, Jamhuri na Zimamoto kwa kushinda mechi zake mbili za kwanza.

Azam FC ilipata ushindi katika mchezo wa kwanza dhidi ya Zimamoto na juzi ikatoka suluhu na Jamhuri, hivyo inatakiwa kuifunga Yanga leo ili icheze nusu fainali.

Bocco anaamini kuwa wanayo kazi kubwa kuifunga Yanga kwani wapinzani wao wapo vizuri na kusisitiza kuwa watajituma kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo.

Mshambuliaji huyo alisema kuwa anaiheshimu Yanga kwani ni timu kubwa na anatarajia mchezo huo kuwa mgumu kwani timu hizo zimekuwa na upinzani kila zinapokutana.

“Tuna kazi ngumu mbele yetu kwani tunakutana na timu kubwa na iliyo na wachezaji wazuri, hivyo itakuwa mechi ngumu. Tunatambua kuwa hata sisi ni timu bora, hivyo hatuna budi kupambana na kushinda mchezo huo,” alisema.

Bocco ambaye hajaonyesha makali kwenye mashindano hayo alisema walitakiwa kuifunga Jamhuri juzi kwani walitengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini hawakupata bao lolote kutokana na kukosa bahati.

“Tulitengeneza nafasi nyingi dhidi ya Jamhuri, lakini hatukuondoka na ushindi, tutarekebisha makosa kabla ya kuvaana na Yanga ili tushinde na kusonga mbele,” aliongeza.

Advertisement