Bosi GSM : Pesa ya kushusha mashine kali Yanga ipo

Thursday April 16 2020

 

By Thobias Sebastian

YANGA wametua kwa straika Mghana na Mnamibia ambao watakuwemo kwenye bajeti ya usajili wa Sh1.5 bilioni iliyoandaliwa kuisuka timu upya kati ya uongozi na wadhamini wao, GSM.

Wachezaji hao ni Mghana Mumuni Shafiu (24), ambaye amezaliwa Mei 11, 1995 (pichani kushoto), na kwa sasa anacheza katika klabu ya Ashanti Gold SC inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini humo.

Mwingine ni Mnamibia, Isaskar Gurirab aliyezaliwa Januari 3, 1998 ambaye hivi sasa anacheza katika timu ya Life Fighters, ambayo alijiunga nayo mwaka 2018.
Mmoja wa wajumbe waliopo kwenye kamati ya usajili ya Yanga aliidokezea Mwanaspoti kwamba, Shafiu wameanza naye tayari mazunguzmo kwa ushawishi wa staa wao, Bernad Morrison kwani anatakiwa na moja ya timu kutoka Romania ambayo kama watashindwa kutoa dau ambalo wao wamelipanga kulitoa wanaweza kumvuta Jangwani msimu ujao.

“Kwa upande wa huyu Gurirab naye tunamtaka, lakini tumeambiwa na timu yake kuwa tayari ana ofa ya Orlando Pirates inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini, kwa maana hiyo kati yetu ambaye ataweza kutoa dau zuri ndiye ataweza kunasa saini ya mshambuliaji huyu,” alisema mjumbe huyo huku akisisitiza kwamba wanaamini ishu zitakwenda freshi kwa vile mchezaji huyo anaangalia masilahi na nafasi ya kucheza mashindano makubwa.

Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msola katika mkutano wake na waandishi wa habari wiki iliyopita kupitia mtandao, alieleza kuwa anafungua milango kwa wapenzi wote wa timu hiyo kwenda kuipa nguvu ili kuweza kufanya usajili wa wachezaji bora ambao watakwenda kuongeza makali ya timu hiyo msimu ujao.

Mkurugenzi wa GSM, Hersi Said aliweka wazi kuwa watafanya
usajili wa wachezaji bora kutokana na bajeti waliyo nayo ili kupata watu ambao watakuwa na tija katika timu hiyo na kufanya vizuri katika Ligi Kuu Bara ambayo wamekosa ubingwa wake misimu mitatu mfululizo.
“Tutasajili wachezaji wazuri ambao watakuja Yanga na tutawawekea mazingira mazuri ya kuwatunza, ili kuona tunafanya vizuri katika mashindano yote msimu ujao na kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi, kwa kwenda kucheza mashindano ya kimataifa msimu ujao,” alisema Hersi huku akiamini kwamba Yanga itatwaa ubingwa wa FA na kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho inayoanza Agosti.

Advertisement

Advertisement