CAF yafuta posho za waamuzi

Muktasari:

  • Ni kwa vyama na mashirikisho Afrika, sasa kubeba mzigo huo kuepuka rushwa

CAIRO, Misri. Tatizo la rushwa kupenya katika soka, limelitikisa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na kuamua kufuta posho za waamuzi kulipwa na vyama na mashirikisho Afrika na sasa posho hiyo italipwa moja kwa moja kutoka CAF kwa waamuzi wanaochezesha mechi inazozisimamia.

Huo ni mwendelezo wa mabadiliko yanayofanywa na CAF katika kuleta mabadiliko ya soka Afrika. Miaka ya nyuma hadi juzi, vyama na mashirikisho ya soka Afrika wanaokuwa wenyeji wa mchezo, walihusika moja kwa moja kulipa posho za waamuzi pamoja na wasimamizi wa mchezo wakiwemo makamisaa.

Taarifa ya CAF iliyotolewa juzi baada ya kikao cha CAF kabla ya kuanza michuano ya CHAN nchini Morocco, ilisema kuwa lengo ni kuvipunguzia mzigo vyama na mashirikisho, lakini kikubwa ni suala la rushwa.

“Hii itasaidia kuondoa viashiaria vya rushwa kwa waamuzi na vyama au mashirikisho ya soka Afrika,” ilisema sehemu ya taarifa ya CAF.

Taarifa hiyo ilisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya ahadi ya Rais wa CAF, Ahmad Ahmad aliyoitoa wakati wa kampeni za kuwania kiti hicho Machi mwaka jana.

Kwa upande mwingine, mpango huo wa CAF kufanya mabadiliko katika eneo la waamuzi, umekuja ikiwa ni mara ya pili katika kipindi kifupi, kwani Desemba mwaka jana CAF, iliifuta Tuzo ya Mwamuzi Bora na zaidi kutokana na suala la rushwa hasa upatikanaji wake.

Kauli ya Madadi, Chama

Akizungumzia hatua hiyo, Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF),Salum Madadi alisema wamepokea uamuzi huo wa Caf kwa furaha kwani utawapunguzia mzigo.

“Watatusaidia sana kwani tunapokuwa na mechi za kimataifa cha kwanza ilikuwa ni kutafuta fedha za waamuzi sasa wakati mwingine hali ya kifedha inakuwa ngumu hivyo mnajikuta katika presha kubwa ya kutafuta fedha kabla ya waamuzi hawajafika.

“Tunamshukuru Rais wa CAF kwa kuliona hili na kutupunguzia mzigo wanachama wake ingawa pia kila kitu kizuri hakikosi changamoto kwani pia licha ya kwamba uamuzi huu ni mzuri lakini inatakiwa fedha za waamuzi zilipwe kwa wakati kwani endapo mwamuzi anacheleweshewa pesa maana yake hawezi kufika sehemu ya kazi kwa wakati,” alisema Madadi.

Madadi alisema uamuzi huo pia usiwe chanzo cha watu wengine kutumia fedha walizonazo katika nchi husika kuwahadaa waamuzi.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF,Salum Chama alisema ni kitu kizuri na kama CAF wameamua basi wao hawana neno.

“CAF ndio wanaopanga waamuzi hivyo kama wao wenyewe wamefanya uamuzi huo wa kuwalipa waamuzi ili kuepukana rushwa ni jambo zuri sana,” alisema Chama.

Michuano ya klabu Afrika

Pia CAF imefanyia mabadiliko kuanza kwa michuano ya klabu Afrika, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho kwamba michuano hiyo itakuwa ikianza Septemba na kumalizika Mei ya mwaka mwingine. Taarifa ya CAF ilisema kuwa michuano ya mwaka huu ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho itafanyika kama ilivyopangwa kuanzia Februari hadi Desemba na baada ya michuano hiyo, michuano mingine itaanza mwaka huu Desemba na kumalizika Mei 2019.

“Tumeifanya hivyo Desemba 2018 hadi Mei kabla ya kuanza ratiba sasa Septemba 2019/2020 na kuendelea,” ilisema taarifa ya CAF.