Carragher aomba radhi kwa ubaguzi

Tuesday October 22 2019

 

London, England. Jamie Caragher amemuomba radhi nyota wa zamnai wa Manchester United, Patrice Evra kwa kitendo cha kumbagua mwaka 2011.
Caragher alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Liverpool waliovaa jezi za kumkingia kifua Luis Suarez baada ya kumfanyia vitendo vya ubaguzi Evra katika mchezo dhidi ya Wigan.
Suarez alimbagua Evra katika mchezo wao Oktoba mwaka 2011 kwenye Uwanja wa Anfield, lakini nguli huyo ameibuka na kusema walifanya kosa ambalo anajutia.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uruguay alifungiwa mechi nane na faini ya Dola 40,000 na Chama cha Soka England kwa kosa hilo.
Carragher na Evra walikuwa wachambuzi juzi usiku na beki huyo wa kati alitumia nafasi hiyo kuomba radhi.
“Naomba radhi hakuna utetezi wa jambo hili, tumefanya makosa kwa kitendo kile. Neno zuri la kusema ni kwamba tulikosoea,”alisema Caragher.
Mbali na wachezaji pia aliyekuwa kocha wa timu hiyo Kenny Dalglish alivaa fulana hiyo iliyokuwa na picha ya Suarez kifuani na mgongoni namba saba.
Evra alisema matukio ya ubaguzi katika viwanja vya michezo hayapaswi kufumbiwa macho kwa kuwa yanadhalilisha utu wa mtu.
“Sikupaza sauti ili Luis afungiwe hapana. Nilitaka kuionyesha dunia kuwa matamshi ya ubaguzi ni sumu katika soka. Unapofanya matukio kama yake pia unaiweka klabu katika hatari,”alisema Evra.

Advertisement