Chama, Kahata waipeleka Simba 16 bora FA

SIMBA imetinga hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho baada ya kuifunga Mwadui  mabao 2-1, mechi hiyo imechezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Ilibidi Simba kusubiri  hadi dakika ya 85 kupata ushindi baada ya Fransic Kahata kufunga bao la pili kwa kichwa akimalizia krosi ya Shomary Kapombe.
Awali mashabiki wa Simba, walimshinikiza kocha kumtoa Kahata dakika ya 67 kwa madai alikuwa akicheza ovyo lakini jeuri ya kocha Sven Vandenbroeck kumbakisha mchezaji huyo uwanjani iliisaidia Simba kupata ushindi huo.
Sven aliamua kutosikiliza kelele za  mashabiki waliotaka amtoe Kahata na badala yake akamtoa kiungo Sharaf Shiboub nafasi yake ilichukuliwa na Ibrahim Ajib dakika ya 73.
Kuingia kwa Ajib kuliichangamsha Simba ambayo ilianza mchezo wa leo taratibu.
Timu zote mbili zilikwenda mapumziko zikiw sare ya bao 1-1 yaliyofungwa na Gerald Mathias Mdamu dakika ya 35 na Clatous Chama dakika ya 45.
Timu hizo ziliporejea mapumziko zilishambuliana kwa zamu lakini Simba walionekana kutafuta zaidi bao la kuongeza kuliko wapinzani wao Mwadui.
Dakika ya 58 wachezaji Jonas Mkude na Meddie Kagere walijikuta wakichanganyana na kushindwa kuipatia timu yao bao kutokana na krosi ya Kapombe.
Mwadui walijibu mashambulizi kupitia Ludovic Evance dakika ya 64 ambaye aliambaa na mpira akapiga shuti lililotoka nje ya lango.