Chama: Simba imepata dawa ya kuiua JS Saoura

Friday January 11 2019

 

By Eliya Solomon, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kiungo wa Simba, Cletous Chama amesema ana uhakika timu hiyo itapata ushindi dhidi ya JS Saoura ya Algeria, mchezo utakaochezwa kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Chama alisema mafunzo ya Kocha Patrick Aussems waliyopewa Zanzibar yalisheheni mbinu za ushindi.

Simba ilirejea jijini juzi ikitokea Zanzibar katika Kombe la Mapinduzi ambapo kikosi cha pili kimekwenda visiwani humo kuendelea na mashindano hayo.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Zambia, alisema wamepata mbinu za kutosha kutoka kwa benchi la ufundi ambazo wameahidi kuzitumia dhidi ya JS Saoura.

“Uwezo wa kushinda mchezo wa Jumamosi ni mkubwa, mafunzo tuliyopata Zanzibar yalikuwa na mbinu nyingi tunazotakiwa kuzitumia,” alisema nahodha huyo msaidizi wa timu ya Taifa ya Zambia.

Chama aliyefunga mabao manne katika hatua ya awali na raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, alisema Simba ina kikosi kipana chenye wachezaji walioandaliwa vyema kupata ushindi.

Simba ilianza kwa ushindi mnono wa mabao 4-1 ilipomenyana na Chipukizi kabla ya kuzifunga bao 1-0 kila moja Mlandege na KMKM.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wasonga mbele katika hatua ya makundi, baada ya kuzing’oa Mbabane Swallows ya Swaziland na Nkana Red Devils ya Zambia.

Advertisement