Chama? msikilize Eymael

VIGOGO wa Yanga wamemvutia waya kiungo nyota Simba, Clatous Chama kuangalia uwezekano wa kumsajili, lakini Kocha wao, Luc Eymael amesema: “Hizo ni blaa..blaa za usajili, tulieni.”

Kocha huyo amesisitiza kwamba amekabidhi majembe kadhaa kwa viongozi waangalie uwezekano wa kuyapata, lakini Chama sio mmoja wao na hayo yanayoendelea mitandaoni ni blaablaa.

Alisema kwamba amesikia kila kitu kinachoendelea, lakini yeye ana utaratibu wake ambao anaendelea nao ingawa hakuweka wazi majina kwa madai kwamba ni mapema.

Chama mwenyewe kupitia akaunti yake ya Twitter juzi jioni alikanusha kwamba hana mpango wa kuondoka Simba na kwamba, bado yupo kwa vile ana mkataba mrefu.

Eymael ambaye ni muwazi kwenye mambo mengi, alisema anadhani ni maigizo tu yanaendelea kuhusu Chama lakini uwezekano wa kumsajili mchezaji huyo msimu ujao kucheza Yanga haupo.

“Kumekuwa na maneno mengi ambayo hata kwangu yananifikia kuwa kuna baadhi ya wachezaji
ambao tunahusishwa nao ikiwemo Chama kutokea Simba, lakini kwangu naweza kueleza
hayo ni mambo tu ambayo huibuka na kupotea kwani hakuna mpango wa kumsajili mchezaji
huyo kwa sasa,” alisema.

“Kweli kuna wachezaji ambao tunawataka na kuna maeneo ambayo nimependekeza, kwa maana
ndio nikaweka sawa kuhusu Chama ni drama tu ambazo zinaendelea huko mtaani
ambazo kwetu hatupo katika mipango nazo,” alisema Eymael ambaye alitakiwa kurudi nchini
leo Jumatano, lakini ameshindwa kutokana na janga la corona.

Mwanaspoti linafahamu Chama alisajiliwa kwa mara ya
kwanza na Simba Julai 2018, kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea timu ya Lusaka
Dynamos ambao ulimalizika msimu uliopita na mara baada ya kumalizika Simba walimuongezea mwingine wa miaka miwili ambao utamalizika mwisho wa msimu wa 2020-2021.

Kwa upande wa Simba kupitia kwa Mkuu wa Idara ya Habari, Haji Manara wao watahakikisha wanaichukulia Yanga hatua kwa kuwa aliyetangaza hivyo ni kiongozi mkubwa ndani ya timu na sio shabiki.

“Angekuwa ni Shabiki tu aliyeongea sisi tungechukilia poa, lakini kuongea makamu mwenyekiti wa Yanga hiyo sio ya kupuuza wamejiingiza matatizoni,” alisema.

Manara alisema, anajua na anatambua Fredrick Mwakalebela anajua vizuri kanuni na sheria kwani mchezaji wao Chama wana mkataba naye na kawaida mchezaji anaweza kufanya mazungumzo na klabu nyingine endapo umebakiza miezi sita.

Alitisha kwamba kitakachowakuta Yanga juu ya suala hilo hawataamini kwani wanaweza kuzuiwa kusajili na pia kupigwa faini, hivyo hawatalifumbia macho jambo hilo.

Manara alisema hata kama wanamhitaji mchezaji huyo, Yanga wanapaswa kufuata taratibu kama wao walivyofanya kumsajili Ibrahim Ajib na Gadiel Michael, na sio kukurupuka tu wakati nyota huyo bado ni mali yao halali.