Chama aeleza ushindani wa namba Taifa Stars - 3

Katika matoleo mawili mawili yaliyopita tulitazama maisha ya nyota wa zamani wa Yanga, Majimaji, Ndovu FC na Pamba, Rashid Idd ‘Chama’. Tunaendelea na simulizi ya mwisho namna beki huyo alivyoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) nchini Nigeria.

Chama anasema alianza kucheza timu ya Taifa ya vijana mwaka 1977 kabla ya kupanda kikosi cha kwanza ambako alipita mikononi mwa makocha mbalimbali nchini.

Anasema licha ya kupata nafasi ya kuitwa timu ya Taifa akiwa mmoja wa vijana hodari waliokuwa wakicheza kwa kiwango bora, lakini hakufua dafu kupata namba katika kikosi cha kwanza kutokana na utitiri wa nyota waliowika enzi hizo.

“Nilianza kucheza timu ya Taifa tangu mwaka 1977 nikiwa Yanga B maana zamani FAT (TFF) walikuwa wanajali timu za vijana na huwezi kuitwa Taifa Stars kama haupo kwenye timu ya vijana na ikitokea hivyo ni mara chache sana,” anasema Chama.

Anasema baada ya kucheza kwa mafanikio Yanga, mwaka 1979 aliitwa kwa mara ya kwanza Taifa Stars kwa mechi za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon).

“Mara ya kwanza naitwa Taifa Stars ilikuwa mwaka 1979 wakati huo nikiwa Arusha na timu ya Mzizima tulipokuja kushiriki michezo ya mashirika ya umma ya Shimuta.

“Kwa bahati nzuri wakati huo timu ya Taifa ilikuwa imeweka kambi mkoani hapa eneo la Duruti ikijiandaa na michuano ya Kombe la Chalenji iliyokuwa inafanyika Nairobi, lakini wakati huo nikiwa pia kwenye timu ya Taifa ya vijana kwa miaka miwili mfululizo. Timu ya wakubwa ilikuwa chini ya kocha Joel Bendera,” anasema Chama.

Anasema baada ya kuitwa kwenye kikosi hicho akaachana na Mzizima iliyokuwa imefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali na kutakiwa Mwanza kuendelea na hatua inayofuta.

Katika michuano hiyo alicheza mchezo wa kwanza dhidi ya Zanzibar kuwania nafasi ya mshindi wa tatu baada ya kutolewa na Malawi kwenye nusu fainali kwa mikwaju ya penalti 5-4, baada ya Kassim Manara kukosa kwa upande wa Tanzania lakini Zanzibar ilitolewa na Kenya.

“Mchezo wetu ulichezwa Uwanja wa Mombasa na ulifanyika kwa siku mbili baada ya kutoka sare siku ya kwanza na kumalizika kwa suluhu na penalti zikawa mabao 5-5, siku ya pili tulitolewa kwa penalti,”anakumbuka Chama.

Afcon 1980

Chama anadokeza Taifa Stars ilikuwa na idadi kubwa ya wachezaji nyota na vijana waliokuwa wakichipukia walikuwa yeye, Willy Kiango na Charles Alberto.

Anasema katika mechi za michuano hiyo alicheza mechi moja dhidi ya Ivory Coast ambayo ilijumuisha idadi kubwa ya wachezaji chipukizi.

Akizungumzia maandalizi ya Taifa Stars itakayoshiriki Fainali za Kombe la Mataifa zitakazofanyika Juni nchini Misri, Chama anasema timu hiyo inatakiwa kupewa maandalizi ya kutosha.

Pia anasema kitendo cha TFF kuwaita wachezaji wa zamani kuwapa neno mastaa wa Taifa Stars waliofuzu fainali hizo ni jambo jema ambalo linapaswa kuendelezwa kwa vizazi vijavyo.

“Nchi nyingi za wenzetu hasa zilizoendelea katika soka zinafanya hivyo ili kuwapa hamasa vijana lakini kwa Afrika imekuwa tofauti na sasa TFF ilikumbuka kwetu,”

“Kitendo kilichofanywa na TFF tuliona kuthaminiwa na bado mchango wetu unatakiwa kwenye Taifa hivyo tulijitahidi kuongea na vijana jinsi ya faida watakayoipata kama watafanikiwa kufuzu Afcon na kweli walitusikiliza na kupata matokeo yaliyokata kiu ya Watanzania,” anasema Chama.

Kikosi cha Stars -1980

Katika kikosi cha Taifa Stars mwaka 1980 alikuwa Athumani Mambosasa, Juma Pondamali, Leopard ‘Taso’ Mukebezi, Daud Salum, Yussuf Ismail ‘Bana’, Mohammed Kajole, Jella Mtagwa, Salim Amiri, Leodgar Tenga, Hussein Ngulungu, Willy Kiango, Mtemi Ramadhani, Juma Mkambi, Omari Hussein, Thuweni Ali, Peter Tino. Mohamed Salim, Mohammed ‘Adolf’ Rishard

Taifa Stars ilikuwa chini ya Kocha Slowmir Work kutoka Poland akisaidiwa na Joel Bendera

Taifa Stars -Afcon 2019

Timu iliyocheza mchezo wa mwisho dhidi ya Uganda na kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa; Aishi Manula, Gadiel Michael, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Aggrey Morris, Mbwana Samatta, Simon Msuva, John Bocco, Farid Mussa, Hassan Kessy, Mudathir Yahya.

Wengine ni Himid Mao, Shabani Chilunda, Thomas Ulimwengu, Mechata Mnata, Feisal Salum na Shiza Ramadhani chini ya Kocha Emmanuel Amunike na Hemed Morocco.

Tanzania imepangwa Kundi C na Senegal, Algeria na Kenya katika fainali hizo zinazotarajiwa kufanyika Juni, Misri. Taifa Stars imekata tiketi baada ya kupita miaka 39.