Chama afunguka yanayoendelea kati yake na Simba Sc

KIUNGO fundi wa mpira wa timu ya Simba, Clatous Chama ‘Mwamba wa Lusaka’ amesema amesikia kila kitu kinachozungumzwa kuhusu yeye kwenye mitandao ya kijamii.

Hata ile ishu ya kwamba amewakaushia mabosi wake kuhusu mkataba mpya ameisikia lakini wanaozungumza hawajui ukweli.

Mzambia huyo ameiambia Mwanaspoti kwamba sio kweli kama amekataa kusaini, isipokuwa ishu ya ugonjwa wa Corona uliofanya Ligi kusimamishwa na wachezaji kupewa mapumziko ndiyo iliyotibua, akidai yupo kwao Zambia akiendelea kupambana kujikinga na ugonjwa huo ulioitikisa dunia kwa sasa.

“Si kweli kama inavyodaiwa nimekataa kusaini mkataba mpya Simba, hayo ni maneno ya watu tu. Ninachoweza kuwaambia msubiri muda sahihi utakapofika, kwani sasa nipo mapumziko nikijifua kivyangu ili kulinda kiwango changu,” alisema akisisitiza kwamba anahitaji mapumziko zaidi na wala Simba hawana presha naye kwavile wanajua ukweli na mashabiki hawapaswi kuwa na wasiwasi.

Kiungo huyo tangu atue Msimbazi miaka miwili iliyopita amekuwa mmoja wa mhimili wa timu hiyo na hasa kazi kubwa aliyofanya na wenzake kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika wakiifikisha Simba robo fainali mbali na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo.

Anakumbukwa zaidi kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa alipoivusha Simba kutinga makundi kwa bao la jioni dhidi ya Nkana FC ya Zambia.