Chama amuweka kikaangoni Aussems

Muktasari:

  • Tathmini iliyofanywa na gazeti hili, imebaini kuwa miongoni mwa wachezaji wanaomponza na kumuweka Aussems katika wakati mgumu ni kiungo Mzambia, Clatous Chama.

KOCHA Patrick Aussems wa Simba amekalia kuti kavu kutokana na mwenendo usioridhisha wa kikosi chake katika siku za hivi karibuni.

Kiwango kisichovutia cha Simba katika mechi zake za hivi karibuni pamoja na kukithiri kwa vitendo vya utovu wa nidhamu kwa wachezaji. Hayo ni miongoni mwa mambo yanayotajwa kuwa chanzo cha Aussem kuwekwa kikaangoni.

Mbali na hayo, kuporomoka ghafla kwa viwango vya wachezaji wa Simba ni sababu nyingine inayotajwa kuwa inaweza kuwa sababu ya Aussems kufungishwa virago.

Tathmini iliyofanywa na gazeti hili, imebaini kuwa miongoni mwa wachezaji wanaomponza na kumuweka Aussems katika wakati mgumu ni kiungo Mzambia, Clatous Chama.

Tofauti na msimu uliopita, Chama wa sasa amekuwa akionyesha kiwango duni katika mechi za Simba jambo ambalo kwa kiasi kikubwa limechangia timu hiyo kutoonyesha kiwango cha kuvutia katika mechi zake.

Takwimu ambazo Mwanaspoti limezikusanya kumhusu kiungo huyo, zinaweza kuwa uthibitisho tosha kuwa anachangia kumuangusha Aussems na Simba

Msimu uliopita, Chama katika michezo tisa ya mwanzoni ya Ligi Kuu, alishindwa kucheza katika michezo miwili tu ya mwanzo kutokana na kutokukamilika kwa vibali vyake vya kuishi na kufanya kazi nchini.

Hata hivyo, katika michezo saba iliyofuata alicheza kwa takribani dakika 565 akifunga mabao mawili na kupiga pasi tatu zilizozaa mabao.

Pia, katika mashindano ya kimataifa, aliichezea Simba mechi mbili kwa dakika 180 dhidi ya Mbabane

Swallows ya Swaziland na katika mechi hizo alifunga mabao matatu huku akipiga pasi mbili zilizozaa mabao.

Lakini hali imekuwa tofauti msimu huu ambapo kiwango cha Chama kimeonekana kupepesuka tofauti na msimu uliopita.

Katika mechi tisa za mwanzoni za Ligi Kuu ambazo Simba imecheza, Chama amecheza katika michezo sita kwa jumla ya dakika 337 tu ikiwa ni tofauti ya dakika 228 huku akifunga bao moja na kupiga pasi moja tu iliyozaa bao vyote akifanya katika mchezo dhidi ya Mbeya City ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-0.

Wakati msimu uliopita akikosa mechi mbili kati ya tisa za mwanzo kutokana na sababu ya kukosa vibali, kipindi hiki mambo yamekuwa tofauti kwani ameshakosa michezo mitatu kutokana na utovu wa nidhamu ambapo mechi mbili zilikuwa dhidi ya

Kagera Sugar na Biashara United hakusafiri na timu kutokana na kutokuwepo kambini wakati kikosi cha Simba kilipoondoka kwenda uwanja wa ndege.

Kiungo huyo pia alikosa mchezo dhidi ya Singida United uliochezwa ugenini Arusha baada ya kutojumuishwa kikosini katika kile kilichoonekana ni kumalizia adhabu yake ya ndani ya klabu hiyo.

Anguko la Chama halijamsibu katika Ligi Kuu tu bali hata mashindano ya kimataifa ambapo ufanisi wake duni umechangia kwa kiasi fulani Simba iondolewe mapema katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Tofauti na msimu uliopita ambapo katika mechi mbili za mwanzo dhidi ya Mbabane Swallows alifunga mabao matatu na kupiga pasi tatu zilizozaa mabao, awamu hii licha ya kucheza kwa dakika zote katika mechi mbili za nyumbani na ugenini dhidi ya UD Songo, hakufunga bao wala kupiga pasi ya mwisho.

Lakini pia changamoto nyingine ya Chama ni kujihusisha kwake na vitendo vya utovu wa nidhamu mara kwa mara msimu huu tofauti na uliopita, tabia inayodaiwa kuchangiwa na urafiki wake wa karibu na Kocha Patrick Aussems.

Kiungo huyo mara kadhaa amekuwa akiripotiwa kutozingatia maadili ya kambi, hivyo kumfanya akose muda wa kutosha wa kupumzika.

Mchambuzi wa soka, Alex Kashasha alisema Chama anasumbuliwa na mambo mawili.

“Chama naweza kusema ameathirika kisaikolojia. Alipokuja nchini mwanzoni ilikuwa ni msimu wake wa kwanza, hivyo pengine alitaka kuthibitisha kuwa anatoka katika nchi yenye kiwango cha juu cha soka lakini pia yeye ni mchezaji mkubwa. Lakini kutokana na sifa alizopewa, akabweteka na kujiona anaweza kuendelea, hivyo pasipo kufuata misingi ya kulinda kiwango chake. Akasahau kazi iliyomleta nchini na kujihusisha na mambo ambayo yameporomosha kiwango chake.”

Kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ alisema Chama anaharibiwa na marafiki wabaya.

“Wachezaji wengi wa kigeni wakija Tanzania siku zote wamekuwa wakiharibiwa na makundi ya marafiki na wachezaji wa Kitanzania. Wanakwenda kwenye ulevi, starehe na uzinzi halafu baada ya hapo wanapotea. Kiwango cha mchezaji ni kama gari, likiwa halina mafuta linazima na hata watu wapige honi vipi haliwezi kwenda mbele.

“Lakini likiwa na mafuta ya kutosha, haliwezi kuzima ndicho kinachotokea kwa Chama kwa sasa,” alisema Julio ambaye aliwahi kuitumikia Simba enzi zake.

“Nina uhakika Chama ndani ya Simba kuna wachezaji ambao ndio wanampotosha na kumfanya asahau wajibu wake kama mchezaji tena wa kimataifa ambao ni kufanya mazoezi na kujitunza. Mbona Kagere (Meddie) anafunga na kufanya vizuri hadi sasa? Ni kwa sababu anaishi katika misingi ya kimpira.”

Julio alimtaka mchezaji huyo kujitambua na kuzingatia mazoezi na maadili ya kambi ili aweze kurudi katika ubora wake.