Chidiebere : Alikuja majaribio Simba,Yanga akaishia kuwa mcheza ndondo maarufu

Mshambuliaji wa Mbeya City Mnigeria Abasirim Chidiebere sio jina geni kwa mashabiki wa soka hasa Kanda ya Ziwa kutokana na uchezaji wake wa kujituma katika timu mbalimbali alizozipitia ikiwemo Stand United, Coastal Union na Pamba.

Lakini nyuma yake kuna mambo mengi ya kusisimua ambayo amelisimulia Mwanaspoti.

SIMBA ,YANGA WALIMLETA

Alifika nchini 2013 kufanya majaribio katika klabu za Simba na Yanga. Alifanya majaribio katika klabu ya Simba kisha baada ya hapo alipelekwa Yanga lakini hakufanikiwa kupata mkataba.

“Sikufanikiwa kusajiliwa na hizi timu mbili ambazo nilikuja kufanya majaribio, niseme ukweli niliumia sana lakini sikuwa na jinsi kwani benchi la ufundi halikunipitisha,” anasema Chidiebere.

KWENYE NDONDO

Chidiebere anasema baada ya dili la kujiunga na timu hizo kuota mbawa akaamua kubaki Bongo, lakini maisha yakawa magumu ndani ya Jiji la Dar es Salaam jambo ambalo lilimfanya aanze kucheza ndondo. Anasema alipata dili mbalimbali za kucheza mechi za ndondo ambazo ziliweza kumfanya apate pesa kwani wakati huo wakala aliyemleta alikuwa amemtekeleza. “Nimecheza ndondo kwa miezi minane, kwa kweli nilipata marafiki wengi sana ambao walikuwa wakinitafutia mechi za kucheza ambazo zilinipa nguvu kidogo kwani nilikuwa napata pesa za kujikimu na maisha magumu nje ya nchi ya watu,” anasema Chidiebere.

Anasema wakati wa pilikapilika za kutafuta maisha jijini Dar es Salaam alikutana na Tabitha Kingolo (mkewe)ambaye walianzisha mahusiano.

Anasema Tabitha alimshawishi waende kuishi Mwanza jambo ambalo alikubali kwani wakati huo mechi za ndondo zilikata na binti huyo ndiye aliyekuwa anamuweka jijini.

“Niseme tu huyu mke wangu amenisaidia sana, kama asingekuwa yeye ningesharudi nyumbani Nigeria na ndio maana chapuchapu niliamua kufunga naye ndoa kwani niliona ana mapenzi ya dhati kwangu.”

Anasema alipofika Mwanza hakuwa na ‘ramani’ kwa kuwa hapakuwa na mechi za ndondo kama ilivyokuwa awali Dar es Salaam, hivyo mkewe aliamua kumtafutia kazi kwa kaka yake mjini Shinyanga.

Anasema shemeji yake alikuwa na kiwanda cha kuchenjua madini mjini humo ambapo alifanya kazi ambayo ilibadilisha maisha yake kwani alikuwa akilipwa mshahara mzuri.

Chidiebele anasema siku moja wakati anafanya mazoezi aliwaona wachezaji wa Stand United wakijifua katika Uwanja wa CCM Kambarage wakati huo wako Ligi Daraja la Kwanza ambapo aliamua kwenda kuomba kufanya nao.

Kocha wa timu hiyo wakati huo, Fulgence Novatus alimkubalia ambapo baada ya mazoezi siku moja mashabiki wakaanza kujaa kumtazama uwanjani.

Anasema kilichokuwa kinawavutia mashabiki ni umbo na kujituma kwake mazoezini jambo lililofanya awe maarufu kwa muda mfupi.

Straika huyo anasema uongozi uliamua kumsajili kwa kumnunulia viatu vya kuchezea huku mashabiki wakijitolea kumpa posho jambo ambalo alilikubali. “Mimi naamini ndiye mchezaji pekee wa Stand United ambaye ninayependwa mpaka sasa pale Shinyanga, na hili lilianza tangu siku ile nimekwenda mazoezini kwao na mashabiki kutaka nisajiliwe kwa gharama zao,” anasema.

RAFU YA MORRIS

Chidiebere anasema Oktoba 12, 2016 hataisahau kwani alichezewa rafu mbaya na beki wa Azam FC, Aggrey Morris ambayo ilisababisha avunjike taya.

Ilikuwa ni katika mchezo wa Ligi Kuu ambao ulipigwa katika Uwanja wa CCM Kambarage ambapo ulimalizika kwa Stand United kushinda bao 1-0.

Anasema licha ya kumsamehe Morris, lakini bado ataendelea kuikumbuka siku hiyo kwani jeraha hilo lilimweka nje ya uwanja takribani miezi miwili.

ATUA COASTAL

Anasema baada ya kutua Coastal Union akitokea Stand United wakati huo alikuwa katika kiwango bora ghafla mambo yakawa magumu kwake.

Mchezaji huyo anasema alishangaa kuanza kupata majeraha ambayo wakati mwingine anakuwa fiti, lakini siku ambayo anapangwa kucheza mechi ghafLa anajikuta anaumwa saa chache kabla ya mchezo kuanza.

“Niseme ukweli kuna wakati niliamua kwenda kanisani kuomba Mungu kwani ile haikuwa hali ya kawaida kwani nilikuwa naumwa katika mazingira ambayo yanatokea kwenye mechi tu, kwa kweli nilikuwa na maisha magumu sana pale,” anasema mchezaji huyo anayependa kula wali na nyama.

LIGI BONGO, AJENGA

Chidiebere anasema amecheza soka katika nchini Zimbambwe na Sudan, lakini hajaona ligi ngumu na yenye ushindani kama ya Tanzania.

Chidiebere anatokea jijini Lagos, Nigeria ambako alianzia soka kwenye kituo cha soka cha Praise King Football na ndiko alikokuzwa kimchezo.

Anaweka wazi kuwa pamoja na jitihada za wazazi kutaka asome, lakini alipomaliza kidato cha nne aliamua kutoendelea na elimu na kujikita katika mchezo wa soka.

Japo anasema bado hajapata mafanikio makubwa kwenye soka, lakini angalau ameweza kujenga nyumba jijini Mwanza ambapo ndipo familia yake ilipo. Mchezaji huyo anasema hana mpango wa kurudi Nigeria.