Chipukizi Azam apelekwa kwa mkopo Nantes ya Ufaransa

Dar es Salaam.Mchezaji chipukizi Azam, Tepsi Evence amejiunga na klabu ya vijana ya Nantes ya Ufaransa kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Tepsi amepata nafasi hiyo baada ya kufuzu katika kliniki iliyofanywa Oktoba 29, 2019 kwenye Uwanja wa Uhuru chini ya usimamizi wa kampuni ya Cambiasso Sport Management wakishirikiana na Rainbow Sport.

Mtendaji mkuu wa kampuni ya Campiasso Sport Management, Twaha Ngwambi alisema Tepsi atacheza Nantes katika timu yao ya vijana chini ya miaka 18, kwa muda wa mwaka mmoja na baada ya hapo ndio watafanya uamuzi.

Ngwambi alisema baada ya mwaka mmoja Tepsi atakuwa na nafasi ya kusajili moja kwa moja na Nantes au kutafuta timu nyingine barani Ulaya.

"Campiasso Sport Management na Rainbow Sport kwa kushirikiana na kampuni ya mawakala wa wachezaji DreamWorld Sports and Entertainment, ndio tutasimamia masuala yote ya msingi ya Tepsi akiwa Ufaransa kwa maana kusoma kwake na mambo mengine muhimu ya kibinadamu kwa muda wote mpaka hapo atakapo sajiliwa," alisema.

"Ninaimani Tepsi atafanya vizuri katika majaribio yake kutokana na ambavyo ameandaliwa na timu yake ya Azam, lakini hata Cambiasso Sport Management, kumpatia mambo ya msingi ya kimaandalizi ambayo alitakiwa kuyafanya kabla ya kuondoka nchini," alisema Ngwambi.

Tepsi alisema anaishukuru timu yake ya Azam, kumpa ruhusa ya kwenda kufanya majaribio hayo ambayo alipata nafasi ya kuonekana kwani bila wao pengine asingeonekana.

“Shukrani nyingine anampa kocha wa Taifa Stars, Ettiene Ndayiragije ambaye alihusika katika kumuandaa kwake na kumpa nafasi hata ya kucheza mechi za kirafiki na timu kubwa ya Azam wakati anaifundisha timu hiyo.