Chirwa: Yondani ni Beki katili kwangu

Muktasari:

Mshambuliaji Mpya wa Azam Fc ya ligi kuu Tanzania Obrey Chirwa amemtaja Yondan kuwa ndiye beki bora anayeweza kumsumbua kwa sasa ana nguvu na anacheza soka la akili hivyo, ni ngumu sana kumpita kirahisi.

ACHANA na Simba na Yanga ambazo zimekuwa zikitawala soka la Bongo, lakini msimu huu Azam ambao walianza kuonekana kama wamepotea vile, wamepania kuzishikisha adabu klabu hizo kongwe.

Ukiachana na Simba ambayo inatajwa kuwa na safu kali ya ushambuliaji ikiongozwa na Emmanuel Okwi, Meddie Kagere, John Bocco na Adam Salama ama Yanga yenye Herieter Makambo, Deus Kaseke, Mrisha Ngassa na Ibrahim Ajibu huko Azam kuna mashine za maana.

Iko hivi. Jana Jumatano mabosi wa Azam FC wamemnasa straika wa zamani wa Yanga, Obrey Chirwa ambaye alitua nchini ili kurejea Jangwani, lakini Kocha Mwinyi Zahera akazuia usajili wake. Wakati Zahera akiweka msimamo wa kutorejea kwa Chirwa, mabosi wa Azam wakafanya kweli na kumshusha Mzambia huyo pale Chamazi na sasa anakwenda kucheza na pacha wake waliokuwa pamoja Yanga, Donald Ngoma. Mbali na Ngoma, Chirwa pia atacheza na Ramadhani Singano (Messi), Enock Agyie, Tafadzwa Kutinyu, Yahaya Zayd na Joseph Mahundi ambao wanasimama jirani na lango la adui.

Chirwa, ambaye amesaini mkataba wa mwaka mmoja, alisema hajarejea Ligi Kuu Bara kizembe bali kufanya kazi na kuziadhibu Simba na Yanga. Pia, ameonya kwa sasa kuna beki mmoja tu anayeweza kumzuia katika kupasia nyavuni pale Yanga, Kelvin Yondani.

Akizungumza baada ya kusaini dili hilo, Chirwa amemtaja Yondan kuwa ndiye beki bora anayeweza kumsumbua kwa sasa ana nguvu na anacheza soka la akili hivyo, ni ngumu sana kumpita kirahisi.

Chirwa aliyeachana na klabu ya No-goom El Mostakbal FC kwa kushindwa kumlipa mshahara alisema:.

“Nimekuja Azam kwa kazi moja kuisaidia kutwaa ubingwa na kufunga mabao mengi ili kuiweka timu mahali pazuri. Sikuja hapa kumaliza soka, ni kama njia tu kwa sababu nina mpango wa kujaribu soka la kulipwa Ulaya. Najua wengi hawafahamu kuwa nimecheza na Okwi klabu moja,” alisema.

Alisema kitu kingine kinachompa jeuri ni kwenda kucheza na Ngoma, waliyekuwa wote Yanga.

“Nimecheza na Ngoma Yanga kwa miaka sita, nina imani tutafanya vizuri tukiwa pamoja hapa, kuna kila kila kitu kinachotakiwa kwa mchezaji hivyo, tutafanya makubwa zaidi,” alisema.

Naye Kocha wa Azam FC, Hans Van Pluijm alisema anafura kubwa kuungana tena na Chirwa kwani, anatambua uwezo wake na ataisaidia Azam kuongeza kasi ya kupasia nyavuni.

“Chirwa ni mchezaji mzuri, anajituma uwanjani na ana kasi. Ni mtu mwenye jicho la kuona goli hivyo ataongeza chachu ya ushindani na kufikia malengo ya kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu,” alisema.

Kwa upande wake, kocha msomi Dk. Mshindi Msolla alisema ujio wa Chirwa ndani ya Azam ni uamuzi sahihi kwani, Ngoma ametoka kwenye majeruhi hivyo bado hana kasi ya mapambano.

“Ngoma kwa sasa anacheza kiujanja ujanja huwezi kumfananisha na yule aliyekuwa moto Yanga, nadhani bado hajapona majeraha yake, Chirwa ni mtu sahihi na atawasaidia,” alisema.

KAZI IPO HAPA

Baadhi ya mashabiki wa Yanga wamepigwa butwaa baada ya Chirwa kutua zake Azam FC wakisema kuwa, mabosi wameacha silaha imekwenda kwa adui huku wakimtupia lawama Zahera, ambaye aligomea Chirwa kurejea Jangwani. “Kwa hilo sipingani naye kabisa, lakini bado tuna mahitaji kwenye eneo la ushambuliaji kwa sababu timu inalinda zaidi hivyo, kama sio ishu ya nidhamu Chirwa angeweza kutusaidia,” alisema Athumani Kihamia.

Naye Ally Mayay alisema Chirwa alistahili kurejeshwa Jangwani kwa hali iliyopo.

“Kwa rekodi ya Chirwa, ni mchezaji ambaye alikuwa akihitajika Yanga tofauti na Azam, lakini nadhani Zahera hakushauri vizuri,” alisema Mayay ambaye ni mchambuzi wa soka nchini.

Hata hivyo, Abeid Mziba na Peter Tino ambao wamedai Yanga ni kubwa kuliko Chirwa, hivyo sio timu ya kubembeleza mchezaji.

“Chirwa haijui historia ya Yanga, iliwahi kuwaacha wachezaji wa kikosi kizima mwaka 1970, wachezaji ambao walikuwa na majina kweli kweli, hata wakitajwa nchi inatikisika akiwamo Sunday Manara, waliondoka na Yanga ikawepo sembuse Chirwa, wacha aende tu Azam,” alisema Mziba.

Alisema klabu haiwezi kumbeleza mchezaji, huku akidai Chirwa hana jambo jipya ambalo anadhani mchezaji chipukizi wa Yanga ataiga kupitia kwake.

Naye Tino alisema: Yanga ni timu ambayo mchezaji akisumbua anaachwa, Chirwa kabla ya kuondoka Yanga angekumbuka namna alivyovumiliwa na kupewa nafasi ahadi akaimarika, lakini yeye ameshindwa kuvumilia kusubiri mshahara.”