Danny Rose, Mourinho wavuragana mazoezini

Muktasari:

Beki nguli wa Tottenham Hotspurs, Danny Rose amemtolea maneno makali bosi wake Jose Mourinho baada ya kumuweka benchi katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Watford, Jumamosi.

London, England. Beki Danny Rose na Jose Mourinho wametoleana maneno makali katika mazoezi ya Tottenham Hotspurs.

Mzozo huo ulianzishwa na Rose ambaye alihoji kitendo cha Mourinho kumuweka benchi katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Watford.

Mourinho alidai alimuweka benchi mchezaji huyo wa kimataifa wa England kwa kuwa alikuwa na jeraha na hakuwa fiti kwa mchezo.

Hata hivyo, Rose alipinga kauli hiyo hatua iliyoamsha hasira na kuanza kumtolea maneno kocha huyo kabla ya mzozo kuibuka mbele ya wachezaji wengine.

Taarifa zilidai kitendo cha nyota huyo kumtolea maneno makali bosi wake kiliwakera wachezaji wenzake ambao wamechukulia tukio hilo ni utovu wa nidhamu.

Pia wapo baadhi ya wachezaji ambao wanadhani mchezaji huyo mwenye miaka 29 hakutendewa haki na Mourinho.

Tukio hilo lilitokea katika mazoezi ya Jumapili jioni ikiwa ni muda mfupi baada ya Spurs kutoka suluhu na Watford ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Vicarage Road.

Rose,  aliyecheza mechi 16 msimu huu, alikuwa akihusishwa na mpango wa kutua Watford kabla ya dili hilo kugonga mwamba. Mkataba wake unamalizika mwakani.